MAUDHUI
Maudhui ya kazi ya fasihi hujumuisha mawazo na
pengine mafunzo mbalimbali yanayowasukuma watunzi mbalimbali kutunga kazi ya
kisanaa (Senkoro, 2011).
Kwa ujumla maudhui katika kazi ya fasihi ni jumla ya
mawazo yote yanayozungumziwa pamoja na mtazamo wa mwandishi juu ya mawazo hayo.
Dhana hii ya maudhui ni pana sana, kwani hujumisha
dhamira, ujumbe, migogoro, mtazamo, msimamo na falsafa ya mwandishi. Ila
kulingana na mwongozo tutahakiki maudhui ya riwaya ya “Mzimu wa Watu wa Kale” kwa kufuata vigezo vifuatavyo;
Ø Muhtasari
wa mtunzi na utunzi wake
Ø Uainishaji
wake
Ø Dhamira
chomozi na
Ø Riwaya
nyingine zinazofanana na riwaya hii ya “Mzimu
wa Watu wa Kale” kimaudhui.
MUHTASARI
WA MTUNZI NA UTUNZI WAKE:
Mohamed
Said Abdulla alizaliwa tarehe 25 Aprili 1918 mtaa wa Malindi Zanzibar.
Alipelekwa chuoni ambako alijifunza kusoma Kurani. Mwaka 1928 mpaka 1937 alisoma
masomo ya msingi katika shule ya serikali, mwaka 1938 alifanikiwa kuendelea na
masomo ya elimu ya sekondari. Baada ya kuhitimu aliajiriwa kuwa ofisa wa afya
ambako alifanya kazi hiyo mpaka mwaka 1958 wakati ajira yake ilipokatishwa.
Baada ya kuachishwa kazi katika idara ya afya alifanikiwa kupata ajira nyingine
ya uhariri wa gazeti la Mkulima.
Alifanya kazi hiyo kwa muda wa miaka kumi, hadi mwaka 1968 pale alipoachishwa
tena kazi ya uhariri katika gazeti hilo. Baada ya kuachishwa kazi hiyo alipata
kazi ya utayarishaji kipindi cha redio kilichoitwa Sadiki Ukipenda katika Sauti ya Unguja.
Mohamed Said
Abdulla alifanikiwa kuoa mke na kupata watoto wawili katika maisha yake. Vile
vile ni miongoni mwa watetezi wakubwa walifanya utetezi katika kuikomboa nchi
ya Zanzibar kutoka mikononi mwa Wakoloni. Na hii ndio ilikuwa sababu ya yeye
kuwa katika hatari ya maisha yake. Miongoni mwa beti zake za kuwatupia watu ujumbe
utakaoweza kuwapotezea nguvu ya kutaka kuinyakuwa Zanzibar. Njama ilianza
kupangwa na wakoloni ili kumuondoa Bwana Msa katika hii dunia. Mohamed Said
Abdulla aliuawa yeye, mke wake na watoto
wake wawili wa kike 1992 katika kipindi cha mapinduzi ya Zanzibar. Hili
lilikuwa pigo kubwa sana kwa Wazanzibari wote kwa kuuawa Bwana Msa katika
mazingira ya kutatanisha (wiki
pedia).
Katika taaluma ya uandishi mchango
wake unaonekana sana katika taaluma ya fasihi kwani aliandika na kuchapisha vitabu
mbalimbali vya fasihi kama vile riwaya, hadithi fupi na tamthiliya. Mohamed
Said Abdulla ameandika riwaya saba ambazo ni;
·
Kosa la Bwana Msa
Mwaka
1958 Mohamed Said Abdulla aliandika riwaya yake ya kwanza ya “Mzimu
wa Watu wa kale” iliyochapwa mwaka 1966. Kutokana na uandishi wa kitabu
hicho alitunukiwa nishani ya juu ya uandishi. Aliandika pia vitabu vingine kama vile Kivuli Kinaishi ambayo ni
tamthiliya na mke wangu ambacho ni kitabu cha hadithi fupi.
Pia alikuwa mhariri na mwandishi wa vitabu tofauti ambavyo
viliinyanyua lugha ya kiswahili katika daraja la juu na kuiongezea umaarufu
mkubwa eneo la Afrika Mashariki.
“Mzimu wa Watu wa Kale” hii
ni riwaya ya kwanza kabisa ya Mohamed Said
Abdulla ambapo
alifupisha jina na kuwa Bwana Msa, pia ndiye aliyekuwa muhusika mkuu katika riwaya
hii ya Mzimu wa Watu wa Kale, riwaya hii inaonesha namna ambavyo Bwana Msa kwa
kipawa alichopewa anagundua kwamba Bwana Ali aliuawa. Katika uchunguzi wake pia
anagudua kuwa Baniani Seti anaipora maiti ya Bwana Ali Sh. 50,000 na
kusafirisha mwili wake hadi kwenye msitu wa Mzimu wa watu wa kale. Spekta Seif
na Najum wanashangaa kutokana na uwezo wa kipekee wa Bwana Msa wa kufukua
ukweli wa mambo.
UAINISHAJI WAKE:
Hii ni riwaya pendwa ambayo inazugumzia juu ya upelelezi, na hii ndiyo sababu inaifanya riwaya hii kuwa katika kundi la
riwaya pendwa kwani riwaya pendwa mara nyingi zinajengwa na dhamira kuu ya upelelezi,
mapenzi, usaliti, na dhamira nyingine zinazozungumzia
mambo yanayopendwa katika maisha ya kawaida na mara zote hutilia mkazo
kipengele cha fani kuliko maudhui. Wahusika wake mara nyingi wahalifu,
wadhulumiwa (waliotendewa kosa), wapelelezi wakiwemo polisi na ni dhahiri kuwa
kama tulivyoona katika riwaya hii wahusika wake wote wana sifa hizo.
DHAMIRA
CHOMOZI:
Dhamira ni mawazo makuu ambayo mwandishi ameafiki
kuifikishia jamii yake. Dhamira kuu katika riwaya hii ni “upelelezi na athari za dhuluma” pia kuna dhamira mbalimbali
chomozi kama vile; hali ngumu ya
maisha na umasikini, uchoyo na ubahili, dhana potofu na imani za ushirikina,
athari za madawa ya kulevya, matabaka, umuhimu wa kuwa na subira, umuhimu wa elimu, umuhimu wa kuthamini lugha
ya Kiswahili, kujitoa mhanga, uvumilivu na kutokata tamaa, ujasiri, suala la dini, nafasi ya vyombo vya
dola, rushwa, athari za kulipiza kisasi na fitina, mapenzi na ndoa na matabaka
Upelelezi
Hali ya kufanya uchunguzi juu ya jambo fulani ili
kubaini chanzo chake, sababu ya kutokea kitu hicho au hata kubaini mambo
mbalimbali. Katika kujadili dhamira ya upelelezi mwandishi anaonesha kuwa suala
la upelelezi sio tu kwa watu wenye majukumu hayo ya upelelezi bali suala hilo
ni kwa watu wote wenye nia ya kujitolea, katika kulionesha hili, mwandishi
anaonesha juhudi za Bwana Msa katika kufanya upelelezi juu ya chanzo cha kifo
cha Bwana Ali, Bwana Msa anajitolea kushirikiana na Najum katika kutafuta chanzo
cha kifo cha Bwana Ali, bila kukata tamaa na hadi mwisho kupata taarifa zote
kuhusiana na kifo chake. Kwa mfano katika sura ya14 kuanzia ukurasa wa 70 hadi
84 Bwana Msa alipokuwa akitoa maelezo juu ya kifo cha Bwana Ali mbele ya
Banyani, spekta Seif na Najumu.
Dhuluma
Hii ni hali ya mtu kuchukua kitu ambacho kilikuwa ni
halali kwa mtu mwingine na kukifanya kuwa chake bila idhini ya mhusuka. Katika
kujadili suala la dhuluma mwandishi Mohamed Said Abdulla anaelezea kuwa dhuluma
ni mbaya sana katika maisha, huweza kumfikisha mtu katika hali mbaya. Mwandishi
anasema;
“Bwana Ali
alitaka kumkimbia mtoto wake Ahmed kwa kudai kuwa si mtoto wake na
kutaka kumuacha kiholela
holela”.Ukurasa wa 78
Mwandishi anaendelea kusemakuwa
“Haki ya mtu haipotei bure, dhuluma haikumfikisha mbali Bwana Ali,
labda
imempakatisha boga tu
makaburini kwa watu wa kale.” Ukurasa wa 78.
Vile vile anaonyesha jinsi ambavyo Banyani na boi
wake (Hamisi) walitaka kudhulumu pesa ambayo Bwana Ali alikuwa ameipokea kutoka
kwao na hivyo anaonesha namna ambavyo walizichukua zile fedha na kurudisha
mfuko kwa maiti na kutafuta namna ya kuificha maiti. Hivyo dhuluma ni mbaya katika maisha na
anaishauri jamii kuachana na tabia ya dhuluma.
Dhamira ndogondogo zilizojitokeza ni kama vile.
Hali
ngumu ya maisha na umasikini.
Mwandishi anaonesha jinsi ambavyo kuna hali mbaya
kwa watu ambao wanaishi eneo la Bwana Msa, anaonesha jinsi ambavyo Bwana Msa alivyo
na maisha magumu kwani hata koti ambalo anavaa limeshonwa kwa sindano ya mkono,
vile vile kanzu ya Bwana Ali nayo pia imeshonwa viraka, pia mwandishi hakuishia
hapo katika kuonesha hali ngumu ya maisha anaonesha pia namna mbavyo nyumbani
kwa Bwana Ali kulivyo anaonesha vibanda viwili ambacho kimoja kilikuwa
kinatumika kwa jiko na cha pili kinatumika kwa kujisaidia haja kubwa lakini
vibanda vyote viwili vilikuwa havina mlango. Mwandishi anasema;
“Vibanda
viwili cha mkono wa kushoto kimefungwa kipande cha gunia mlangoni
kinachoningi’nia katikati hakimzuii mtu kuona kwa
juu wala kwa chini na kumsitiri
aendaye haja huko msalani, kibanda cha pili kilikuwa
jiko , nacho kilikuwa wazi na
mtu aliweza kuona mabonge ya
udongo matatu manne yaliyotumika kuwa majifya
navijinga viwili vitatu vilivyo
kwisha tumika ukurasa wa 12”
Huu ni mfano mzuri katika
kuonesha hali ngumu ya maisha. Katika jamii yetu pia kuna hali ngumu ya maisha
tunaona watu wengi sana katika jamii wanakosa sehemu ya kulala, wanalala njaa
kwa kukosa chakula. Hivyo ni jukumu letu kama wanajamii kufanya kila
liwezekanalo kuondokana na hali ngumu ya maisha, ikiwa ni pamoja na kufanya kazi
kwa bidii na kuacha uvivu.
Uchoyo
na ubahili
Katika kujadili dhamira hii, mwandishi anaonesha namna
ambavyo uchoyo na ubahili umetawala kwenye mioyo ya watu. Katika jamii yetu
amemtumia Bwana Ali kama mfano wa watu bahili ambao tunaishi nao kila siku, mwandishi
anasema;
“Bwana Ali alikuwa akishtaki njaa kila baada ya saa mbili, na hainyamazi
mpaka ashibe, lakini alivyokuwa yeye ni mtu bahili
sana hakuweza kujilisha kwa
namna tumbo lake lilivyohitaji; kwa hiyo ubahili
wake ulimwonyesha dawa rahisi
sana- kutafuna tambuu na kumeza
mate”
ukurasa wa 7.
Mwandishi anaendelea kuonesha jinsi ambavyo Bwana
Ali alikuwa pia mchoyo katika uk.7 mwandishi anasema; “alikuwa mtu mwenye choyo na tamaa, hasa katika masaala ya mali”.
Hivyo ni wazi kuwa hata katika jamii yetu kuna watu wachoyo na wenye tamaa
hivyo ni vyema tukaachana na tabia kama hizo, katika kuonyesha hili mwandishi
amemtumia Ahmed Ali ambaye alikuwa ni kijana wa Bwana Ali lakini hakupendezwa
na ubahili wa baba yake, katika ukurasa wa 8, mwandishi anasema;
“Kwa hakika alikuwa akifikiri, kwa maana ubahili wa baba yake ulimkaa
kama donge kubwa la uchungu rohoni mwake…., ubahili wa baba yake hausemeki”.
Hivyo basi mwandishi anatuonesha jinsi ambavyo
ubahili ulivyo hata unaleta vikwazo kwa watu tunaoishi nao na hivyo tunapaswa
kuachana na ubahili, uchoyo pamoja na tamaa.
Umoja
na mshikamano
Umoja na mshikamano ni kitendo cha kushirikiana
baina ya mtu na mtu, kundi na kundi au baina ya pande mbili ili
kufikia/kufanikisha lengo au jambo llilokusudiwa. Katika kitabu hiki mwandishi
anatuonesha umoja na mshikamano baina ya Bwana Msa na Najum, hii inaonekana
dhahiri pale wanapoungana kwenye suala la kutafuta chanzo cha kifo cha Bwana
Ali. Wanafanya kazi hiyo kwenye mazingira magumu kwa pamoja ili tu kujua Bwana
Ali alipo na kwa nini hakurudi nyumbani kama kawaida yake. Bwana Msa pamoja na
Najum wameshirikiana sana kwa pamoja na kwa umoja kuanzia mwanzo wa upelelezi
hadi mwisho wa upelelezi kama inavyoonekana ukurasa wa 6 hadi ukurasa wa 86 katika hii riwaya. Pia
kuna ushirikiano baina ya Bwana Msa, Najum, na spekta Seif. Hii inaonesha wazi
katika hatua za upelelezi waliokuwa wakifanya, spekta Seif aliwapa ushirikiano
wa hali ya juu Bwana Msa pamoja na Najum katika kujua sababu ya mauaji ya Bwana
Ali, hii inajidhihirisha wazi katika sura ya 10 ukurasa wa 51.
Katika jamii yetu suala la umoja na ushirikiano
linaonekana kupungua kwa kiasi kikubwa kwani jamii nyingi zimeshindwa kuendelea
kwa sababu hakuna umoja na ushirikiano miongoni mwa wanajamii pia hakuna umoja
na mshikamano kwenye baadhi ya ndoa, wafanyakazi, viongozi na hata kwa
wanafunzi. Mfano mzuri ni wanafunzi wa vyuo vikuu wengi wao wamekuwa wazembe na
wategeaji katika suala zima la kufanya kazi ambazo zinatolewa katika makundi na
kusababisha kazi nyingi kuchelewa kukusanywa kwa muda husika.
Hivyo basi ni vema tukajenga tabia ya kushirikiana
kwa pamoja ili kuleta maendeleo katika jamii kwani umoja ni nguvu na utengano
ni udhaifu na pia umoja ni nguzo kuu ya maendeleo ya jamii kwa kila nyanja.
Uzembe
kazini/ kutokuwajibika.
Mwandishi anaonesha jinsi ambavyo watu huwa ni
wazembe katika kazi zao, hii inaonekana pale ambapo askari Kalungu anaposinzia
katika eneo la kazi stesheni badala ya kuwajibika kazini kwake ukurasa wa 51.
Mwandishi anatuonesha mfano mzuri hata kwa jamii tunayoishi watu wengi ni wazembe
kazini kwao badala ya kufanya kazi hukalia mambo yasiyowahusu kupiga umbea au
hata wengine kusinzia kazini kwao na kurudisha nyuma ufanisi wa kazi yao na
kusababisha makosa mbalimbali kazini kwao. Hivyo ni vyema tukaachana na uzembe
na tuwajibike wakati tungali kazini kwetu.
Ujasiri
Ujasiri ni hali ya kuthubutu kutenda jambo ambalo ni
gumu yamukini linaloweza kusababisha madhara makubwa kwa binadamu husika.
Katika riwaya hii ya“Mzimu wa Watu wa
Kale” suala la ujasiri linajitokeza pale ambapo Bwana Msa na Najum wanathubutu
kuingia mzimuni, wanaazimia kuingia mzimuni japokuwa wanashuhudia maajabu
mbalimbali. Mfano mzuri mwandishi mwenyewe anasema;
“Ndani mlikuwa na kiza kama uwanda wa ahera. Kiza
kilikuwa kimetapakaa kinavuja.
Sauti
za komba na mabundi-wasiojua kwa sababu ya kiza kilichozagaa”. {U kurasa wa
26.}
Vilevile mwandishi anaendelea kusema katika ukurasa
wa.33
“Ndani kama tulivyosema, kiza tororo! Hapana mmoja aliyemuona
mwenziwe
Kunatisha!”.
Hivyo tunaona hali
halisi ya mzimuni ilivyokuwa inatisha hali ambayo ingepelekea Bwana Msa na
Najum kukata tamaa mapema kwa sababu kunatisha lakini kutokana na ujasiri waliokuwa
nao hawakukata tamaa bali waliendelea kuingia mzimuni na hatimaye waliweza kubaini
kifo cha Bwana Ali.
Katika jamii suala la ujasiri linaonekana maeneo
mbalimbali kwa watu baadhi ambapo ujasiri wao umepelekea kuwepo na ufanisi
katika mambo mbalimbali. Mfano, kuwepo kwa viongozi jasiri katika vyama vya
siasa kumepelekea kufahamika kwa mambo mbalimbali yaliyokuwa ni ya siri, tena
ambayo jamii haikuyafahamu. Mfano mzuri ni kuwepo kwa Richmond na fedha ya rada
kumetokana na viongozi jasiri waliothubutu kujitoa muhanga kuibua siri ya
vigogo wa serikali.
Uvumilivu
na kutokata tamaaa
Hii ni hali ya ustahimilivu wa hali ya juu ambapo mhusika
anapambana na mambo makubwa ya ajabu yanayo katisha tamaa lakini yeye anaonesha
msimamo wa kukabiliana nayo na kutokubali kushidwa.
Katika riwaya hii mwandishi Mohamed Said Abdulla
amewatumia wahusika ambao ni Bwana Msa na Najum ili kutuonesha kuhusiana na
suala la uvumilivu na kutokata tamaa. Bwana Msa pamoja na Najum wanaonekana
kutokata tamaa katika kupeleleza chanzo cha kifo cha Bwana Ali na hata mwisho
walipobaini chanzo cha mauaji ya Bwana Ali. Tunaona dhahiri katika ukurasa wa 26,
27, na 28 kuwa safari ya kuelekea kwenye kichaka cha Mzimu wa watu wa kale
ilikuwa ni ngumu sana lakini Bwana Msa na Najum walijitahidi bila kukata tama,
kunaonekana kulikuwa na umande ambao uliloanisha suruali zao pia tope la kule
kileleni lilikuwa linateleza lakini walijitahidi sana lakini kikubwa zaidi waligongwa
na vizuu hadi kuzimia na kujeruhiwa lakini hawakukata tamaa bali waliendelea na
kazi yao mpaka mwisho.
Katika jamii yetu watu wengi wamekuwa hawafikii
malengo na matarajio yao kutokana na kukata tamaa, suala la uvumilivu kwa walio
wengi halipo na ndio maana mtu anapokumbana na kikwazo tu hukata tamaa na
kutoendelea na kile ambacho alikuwa akikifanya. Mwandishi anatuasa tuwe na moyo
wa kuweza kuvumilia mambo kama ilivyo kwa Bwana Msa pamoja na Najum ili kuweza
kufanikisha yale ambayo tumeyakusudia kuyatenda kwani katika kufanya jambo
lolote lile ni dhahiri kuwa kuna vikwazo na ugumu wake, hivyo moyo wa kuvumilia mambo unahitajika.
Kujitoa
mhanga
Katika riwaya hii ya mzimu wa watu wa kale tunaona
kwamba Bwana Msa akishirikiana na Najum walijitoa muhanga kuingia katika
kichaka kiitwacho mzimu wa watu wa kale ambacho ni kichaka hatari nia ikiwa ni
kumtafuta Bwana Ali ambaye hakurudi nyumbani kwake na hivyo Bwana Msa anasema;
“Mimi na
wewe Najum, hatudhuriki kwa mzimu maana sote wawili tunajua kwamba vivuli
vya
maiti havimjii mtu ila katika ndoto,……………….Bismillah, twende zetu” katika
(ukurasa wa 24).
Mbali na hatari ya kufa
katika kichaka kile, lakini waliazimia kukabiliana na lolote lile ambalo
lingeweza kutokea ili wafanikishe suala
zima la kumtafuta Bwana Ali, Ukurasa wa 25-27 tunaona kwamba Bwana Msa na
Najum, wanaendelea na safari yao na makwazo mfano Najum anapigwa kumbo la nguvu
na vizuu wa watu wa kale lililomfanya azimie.Na anapozinduka wanaendelea na
safari yao.
“ile hali ya kuingia katika mzimu
wa watu wa kale ilikuwa kujitoa sadaka kwa chochote
kile ambacho kingetokea, walikuwa
tayari”
Pia katika ukurasa wa 32”Ndani ya mzimu” tunaona
kwamba kuna giza totoro! Hapana mmoja kumwona mwenziwe ni kunatisha, lakini
walipiga moyo konde na katika ukurasa wa 38, mwandishi anaeleza kuwa Bwana Msa
na Najum walimwona Bwana Ali akiwa makaburini na amekatwa kichwa huku akiwa
amenyoosha miguu yake na kupakata kichwa chake, Bwana Msa anasema;
“Njoo, Najum! Njoo umtazame Bwana Ali kakatwa kichwa”
Bwana Msa na Najum pia walijitoa mhanga katika
kuhakikisha kwamba muuaji ambae alihusika na kifo cha Bwana Ali anapatikana,
hivyo walijitoa mhanga kufuatilia chanzo na muhusika ili naweze kufikishwa
katika sheria na hivyo waliamua kuripoti tukio polisi ili waweze kusaidiwa
katika utafiti wao. Mfano katika uk.48 tunaona kwamba Bwana Msa anamwambia
Najum kuwa waende kutoa taarifa polisi ili wasaidiwe, anasema;
“Unajua
we, sasa twende polisi tukapige ripoti”
Na katika ukurasa wa 49 – 50, mwandishi anaeleza
jinsi Bwana Msa na Najum walipofika
stesheni ya polisi na kutoa maelezo yao kwa Inspekta Seif juu ya kifo cha Bwana
Ali ambae alitoka alasiri jana na hakurudi kulala na kugundulika kuwa kauawa.
Na katika uk.80, tunaona kwamba kutokana na kujitoa
muhanga na nia yao kubwa ya kumpata muuaji, na kufuatilia chanzo cha kifo cha
Bwana Ali, mwandishi anasema muuaji alipatikana na keshakamatwa ambae ni
Mwarabu mgeni na sababu yake alisema ya
kuwa alimharibia nyumba yake alipokuwa Kongo maana alikuwa na pesa nyingi za
kuchezea na kufisidia wake wa watu.
Katika jamii yetu kuna watu wengi hujitoa mhanga kwa
ajili ya kutaka kufanikisha mambo ambayo huwa wameyakusudia. Hivyo mwandishi
anatuonesha kuwa kujitoa mhanga ni njia mojawapo ya kuweza kuyafikia malengo
ambayo tumeyakusudia na ili kufanikisha malengo, lazima tusikate tamaa,
tuvumilie na tujitolea mhanga ili tuweze kuyafikia malengo.
Umuhimu
wa kuthamini lugha ya kiswahili.
Hii ni dhamira nyingine ambayo imejitokeza katika
riwaya hii. Mwandishi kwa kumtumia mhusika mkuu Bwana Msa ili kutuonesha ubora
wa kuthamini lugha yetu na umuhimu wa kutumia kiswahili sanifu katika
mazungumzobadala ya kuiga lugha nyingine. Bwana Msa anasema;
“Lakini katika maelezo yangu
nitatumia Kiswahili change mwenyewe, sitaiga Kiswahili
cha kibaniani…” katika uk.70.
Lugha ya baniani ni lugha ambayo haina lafudhi na
matamshi ya kiswahili mfano mwandishi anasema;
“Banyani
aliruka, kashtuke, kisha akajikaza akasema, ile biashara bana: mi wapi
Weza pigana fanga, bana
watu naweka rahani bana” ukurasa.66.
Hii inaonesha jinsi
ambavyo mwandishi amekusudia kuasa jamii kutokuiga lugha mbalimbali au kuchanganya
lugha na hatimaye kuharibu lugha husika. Katika jamii yetu suala la kuchanganya
lugha linatumiwa na wajunzi wa lugha na hata pia wazawa wa luha husika hii
hupelekea kudunisha lugha husika na kuibuka kwa lugha ambazo sio rasmi au
sanifu mfano mzuri tunaona watu wengi wakichanganya Kiswahili na kiingereza
jambo ambalo linasababisha upotoshaji wa lugha sahihi, mfano utamsikia mtu
akisema nilikuwaroom, nigei kitabu, lipa buku tusepe, nimepoteza mane, michogo
haijakaa freshi, na maneno mengine mengi ambayo yanapotosha lugha husika. Hivyo
mwandishi anatukumbusha kuithamini lugha yetu na kuachana na dhana potofu,
ambapo wengi huamini kuwa kuchanganya lugha ni ujuzi wa lugha na pia wengine
huona kuwa ni usomi, lakini tukitumia lugha ipasavyo tutaidumisha na kuikuza.
Rushwa
Hii ni hali ya kupokea au kutoa kitu ambacho
hukustahili kutoa au kupewa ili kusudi uweze kupata, kupewa au kufanyiwa jambo
ambalo ni kinyume na utaratibu maalumu. Rushwa kupotosha haki za binadamu na
hata kusababisha ukosefu wa ukweli.
Katika riwaya hii suala la rushwa limejitokeza pale
ambapo Bwana Msa anaposilia kuhusu Seti kumshirikisha boi wake kumpa kitu
kidogo ili kuficha siri ya Seti ya kuchukua sh. 50,000 kwa Bwana Ali alizompa
kwa kumuuzia shambaa baada ya Ali kuwa ameuwawa kwa kukatwa panga na mwarabu.
Bwana Msa anasema kuwa;
“Ulimpa boi wako shauri
hili, na ukamrubuni kwa chochote naye akakubali” hapa
inaonekana wazi kuwa
alipewa hongo ili kuficha siri hivyo” katika uk.74.
Katika jamii suala la rushwa limeenea sana na
limepelekea ukosefu wa haki kwa wanajamii na pia kuwanyima walengwa uhuru binafsi
wa kusema ukweli. Mfano mzuri mtu hushindwa kusema ukweli au kutoa ushahidi wa
ukweli kutokana na rushwa ambayo amepewa hasa katika mahakama mbalimbali, au
hata kwenye ofisi mbalimbali.
Dhana
potofu na imani za ushirikina.
Mwandishi anaonesha namna ambavyo watu huamini
uchawi na namna gani ambavyo mtu akiugua kwa muda mrefu watu husema karogwa
mfano mzuri ni Kipwerere mabaye baada ya kuugua sana watu waliamini kuwa;
“Karogwa na wachumba waliomhitaji wakamkosa, wengine wakaamini kuwa
chanzo
cha ugonjwa wake umedhurika
katika kile kichaka kiitwacho “muzimu wa watu wa
kale” alipokuwa akipita, siku hizo bado kigoli na
huku anakula ndizi ya kipukusa; kwa
hiyo shetani wa muzimuni
alimshika na kumpanda kichwani, wala hatamtuliza na kumpa
nafasi ili apate chano ya ng’ombe Uk11”.
Mwandishi anaonesha jinsi ambavyo wazee waliamini
kuwa mtoto wao kasibika na shetani, hivyo mwandishi anatutaka tuondokane na
imani potofu kwani huchangia kukwamisha maendeleo na kurudisha nyuma uchumi wa
taifa. Mwandishi pia anaonesha jinsi ambavyo watu wanachangishana pesa kwa
ajili ya kununua ng’ombe wa kutambikia mzimu ili ipate kulala na watu wa
kiamboni wapate kutulia, pia anaonesha namna ambavyo watu wana dhana potofu juu
ya nyani na kima wanaoishi katika mzimu wa watu wa kale hawapigwi kwa sababu
jamii inaamini kuwa ni vizuu vya watu wa ke, hii ni imani potofu. Pia tunamuona
Najum na Bwana Msa jinsi wanavyo usujudia mzimu kabla ya kuingia ndani. Hii
huhusiana na imani za kishirikina, na hata katika jamii yetu kuna mambo mengi
hutendeka kwa ajili ya wanajamii kushikilia mila au imani fulani na kudumaza
maendeleo, hivyo ni vyema tukaachana na imani zisizofaa.
Matumizi
ya dawa za kulevya
Mwandishi anaonesha namna ambavyo matumizi ya madawa
ya kulevya yalivyo na madhara hasa kwa yule anayetumia madawa hayo, mfano mzuri
anoonesha uvutaji bangi unavyochangia watu kuchomana visu na hata kupelekea
vifo vya watu mbalimbali, mwandishi anaseama;
“Boi wa Banyani
(Hamisi) anavyovuta bangi anavuta bangi ambazo humpelekea
kupigana visu” uk.62.
Pia mwandishi anamuonesha Sufra ambaye ni mvutaji
bangi na ambaye amewahi kuwauuwa Sharifu na mwanaye. Mwandishi anasema;
“Sufra ni mvuta bangi maarufu, ana duka kubwa
la tambuu na sigara. Sufra ndiye
aliyewaua Sharifu
na mwanae kwa kuwachoma kisu” uk 63.
Hivyo mwandishi anaonesha madhara yanayotokana na
kuvuta bangi na tumbaku, anaonyesha kuwa uchafuzi wa fizi ni mojawapo ya athari
zitokanazo na uvutaji tumbaku. Uk.67 mwandishi anasema;
“Banyani fizi zake zimechafuliwa na tumbaku anyotumia”.
Katika jamii yetu, suala la madawa ya kulevya
limekuwa likipingwa vita kila kunapokucha kwani limeonekana kukithiri sana.
Hivyo ni jukumu la kila mmoja wetu kuliangalia na kulikemea, kwani tunaona kuwa
matumizi ya madawa ya kulevya yana madhara kwa jamii na hata kwa watumiaji
wenyewe.
Matabaka
Hii ni dhamira mojawapo ambayo mwandishi
ameizungumzia katika kitabu hiki cha “Mzimu
wa Watu wa Kale” mwandishi anaonesha kuwa;
“‘njia kuu ya magari’ iliigawa Baraste katika pande mbili kubwa
kubwa; upande mmoja
kuna machunga mazuri
yaliyochanganyikana na kichaka kiitwacho ‘mzimu wa Watu wa
Kale’ na kuishia karibu na
nyumba ya Bwana Ali, na upande wa pili ndiko kwenye
maskani ya watu, makonde yao,
maduka, soko na stesheni ya askari.” uk.6.
Hivyo kuna matabaka kati ya watu wenye uwezo wa hali
ya juu kimaisha na watu wasio na
uwezo kwani tunaona wazi kuwa watu wasio
na uwezo wanaishi Kikwajuni na sehemu za mnazi mmoja lakini watu wenye uwezo wa
juu, wenye maduka, waliishi sehemu za Baraste.
Katika jamii yetu pia suala la matabaka lipo,
matabaka honekana kuanzia sehemu tunayoishi, makazi na hata kwenye utawala
tulionao. Matabaka ni mabaya na ni vema tukawa na umoja na mshikamano tukaondoa
matabaka yaliyopo ili tuweze kupata maendeleo.
Mapenzi
na ndoa
Katika kujandili suala la ndoa mwandishi anaonesha
kuwa kuna ndoa ya kulazimishwa au ndoa ya kuchanguliwa mume. Mfano mzuri ni
kipwerere ambaye anaolewa na mtu mbaye sio changuo lake (Bwana Ali) kwani Bwana
Ali alimuoa kipwerere kutokana na mali alizokuwa nazo baada ya kuelewana na
wazazi wake tu lakini kipwerere mwenyewe hakumpenda Bwana Ali kama mwandishi
anavyosema;
“Lakini sijui kwa sababu ya
mali maana ukiwa na mali huko sio bahati, wote wale
waliokuwa wakimkamia
kumwoa walirushwa wasimpate, akaja Bwana Ali…”uk.9.
Kutokana na mapenzi haya yasiyo ya dhati kipwerere
aliishi kwa Bwana Ali pasipo kupata furaha ya ndoa kwa muda wa miaka kumi na
hivyo kuonekana muda wote akisononeka kama mwandishi anavyosema;
“miaka
kumi tena sasa tangu kipwerere yuko kwa mumewe lakini muda wote huo
alikuwa akisononeka tu,
mgonjwa si mgonjwa, mzima si mzima…” uk.9-10.
Haya maelezo yanasawiri vyema jinsi kipwerere
alivyokosa raha akiwa kwenye ndoa. Aidha yote haya yalisababishwa na ubahiri wa
mumewe (Bwana Ali) kiasi cha kutokumjali mke wake hata katika masuala muhimu
kama vile matibabu kama asemavyo mwandishi;
“na kwa hiyo kila dhofu lihali likizidi kumkondesha kipwerere, wazee
wake humshika
mumewe Bwana Ali, atoe
ngombe mmoja ili apewe chano mtoto wao, apate kupumzika,
lakini Bwana Ali huzidi
kuwapa ahadi za mbele tu, mwaka baada ya mwaka mpaka leo
uk.10”.
Kutokana na ubahiri huo kunasababisha kukithiri kwa
ugonjwa wa kipwerere hivyo kuthibitisha kuwa Bwana Ali hakuwa na mapenzi ya
dhati kwa mkewe. Kwa hiyo mwandishi anaonesha dhahiri kuwa hakukuwa mapenzi ya
dhati kati ya Kipwerere na mumewe Bwana Ali.
Hivyo basi katika jamii yetu ya leo ni dhahiri kuwa
hakuna mapenzi ya kweli baina ya wanandoa kwa sababu kuna udanganyifu mwingi
katika ndoa na pia ndoa nyingi hazidumu kutokana na kuosekana kwa mapenzi ya
dhati baina ya wanandoa. Hivyo basi ni vyema tukiwa na mapenzi ya dhati kwa
wake zetu na waume wetu ili kusudi tudumishe ndoa na uaminifu katika familia na
jamii kwa ujumla.
Athari
za kulipiza kisasi (kuwa na fitina).
Kisasi ni hali ya kumfanyia mtu kitu kibaya kwa
ajili ya kulipa mabaya ambayo aliwahi kukufanyia. Mfano katika riwaya ya “Mzimu
wa Watu wa Kale” Bwana Ali ameonekana kuwa alikuwa anaishi Kongo pamoja na
Waarabu. Bwana Ali alikuwa na mali nyingi ambazo alidhulumu kutoka kwa Waarabu
na kukimblia Unguja. Baada ya muda Bwana Ali alisikia kuwa moja kati ya Waarabu
hao ameingia Unguja, Bwana Ali aliuza mali zake zote kwa bei ya chini ya
shilingi 60,000 ili aweze kukimbia. Mfano mwandishi anasema;
“Mimi
Ali bin Boman,nakiri kuwa nimestakabadhi kwa Seti B. Sumatra, shs.50,000/- leo
na zimebaki 10000 nita
stakabadhi kesho mjini” katika uk 30.
Baada ya kuuza mali Bwana Ali ameonekana kuuawa kwa
kukatwa kichwa uk73. Vivyo hivyo
katika jamii zetu za sasa kuna watu wenye tabia za kulipiza visasi kwa mabaya
wanayotendewa. Kutokana na tendo hilo mwandishi anatufundisha kuwa si vizuri
kulipa visasi.
Nafsi
ya vyombo vya dola
Vyombo vya dola ni pamoja mahakama, serikali, na
polisi. Vyombo vya dola hushirikiana na wananchi kusaidiwa wanapopatwa na
matatizo. Katika riwaya hii nafasi ya vyombo vya dola inaonekana kwani tunaona
Inspekta Seif na askari Chombeko wanaambatana na Bwana Msa na Najum kufanya
utafiti ili wajue ni nani hasa amehusika katika mauaji ya Bwana Ali.
Wanashirikiana hadi kugundua kuwa aliuawa na mwarabu mgeni wa Mmanga kutoka
kongo mbaye alimkata panga shingoni na kutenganisha kiwiliwili na kichwa, pia
katika kuangalia nafasi ya vyombo vya dola tunaona Inspekta Seif akimwambia
Bwana Msa aichie polisi uchunguzi katika kupima ni hatua ngapi kutoka kichwa
kilipoa hadi maiti ilipo kama anavyosema uk.
“mfano kutoka katika kitabu”
Katika jamii tunaona wazi kuwa serikari nayo ina
jukumu la kusaidiana na wanancihi wake katika kutatua matatizo mbalimbali pia
kuhakikisha usalama wa kila raia ili kujenga taifa lenye umoja na mshikamano.
Hivyo ni jukumu letu kutambua nafasi ya vyombo vya dola na kushirikiana nao ili
kuondoa na kutatua matatizo yalipo katika jamii.
Suala
la dini
Katika riwaya hii tunaona kuwa kuna dini iitwayo
kibanyani ambapo haimrusu mtu kuua maana baada ya Bwana Msa kuelezea ukweli juu
ya kifo cha Bwana Ali, Banyani anafurahi kutolewa kutoka dhambi ya mauaji ya
Bwana Ali, mwandishi anasema;
“diyo bana iyo bana kwa hakika kuwa katika dini ya kibanyani, zaidi
kuliko katika dini
nyinginezo ni dhambi zisikuwa
na mfano”
uk74
Kwa hiyo tunaona hii dini inakwenda kinyume na
inatenda mambo mengine kinyume kwani tumeona kuwa katika dini hii ni dhambi
zisizokuwa na mfano, kwa hiyo mwandishi anashauri kuwa na dini nyingine lakini
sio hii dini ya kibanyani dini ambayo hutoa kafara juu ya mzimu. Katika jamii
yetu leo tunaona kuwa dini nyingi sana zimeenea sana, na kila mmoja huamini
kuhusiana na dini anayohudhuria.
Mila
na desturi
Mila na desuri katika riwaya hii huhusu jamii ya watu wa kiamboni na
huendeshwa kwa kufuata utaratibu unaohusisha utoaji wa kafara na matambiko ya
mizimu katika mzimu wa watu wa kale. katika kutoa kafara, watu huchanga pesa
ili kununua n’gombe wa kuchinja ili mizimu iweze kutulia. Mwandishi anasema;
“Mpaka uje wakati na wao waone ni mno tena, mizimu haitulii mpaka
itambikiwe”
Hata kwenye jamii yetu kuna watu hufanya kafara
mbalimbali ili kufanikisha mambo mbalimbali. Hivyo basi mwandishi anaonesha
namna ambavyo tunakosa maendeleo kwa kutumia pesa kwenye mambo ya kiimani.
Hivyo ni vyema tukaondokana na mila zilizopitwa na wakati.
Umuhimu
wa elimu
Elimu ni maarifa, ujuzi au mwelekeo anaoupata mtu
kutokana na chanzo kimoja hadi kingine, kwa njia ya kusoma, kusimuliwa,
kufundishwa au hata kuona. Elimu ndio chombo kikuu cha ukombozi wa mwanadamu
dhidi ya unyonyaji, umasikini, rushwa na hata ukandamizaji.
Katika hii riwaya kumejitokeza elimu za aina
mbalimbali mfano mwandishi anasema;
“Bwana Msa alikuwa na elimu za
siri za aina mbili, yaani elimu ya ndoto na elimu ya na
kivuli”
Ambapo Bwana Msa alitumia elimu ya ndoto katika
kuona mambo yaliyo mbali na upeo wa macho ya kawaida ya mwanadamu mfano kuhusu
kifo cha Bwana Ali. Pia alikuwa na uwezo wa kufasili vivuli, kusoma kiarabu
japokuwa hakuwa mwarabu (uk.28). Pia Najum naye alikuwa na elimu na ndio maana
aliweza kucheruka juu ya karatasi iliyoonesha kuwa haina sahihi na tarehe kuwa
sio halali, uk.30. Pia umuhumu wa elimu inaoneshwa uk.40, uk.52 na uk.54 katika
toleo la mwaka 1971. Hivyo mwandishi anaonesha kuwa elimu huleta maendeleo na
bila elimu hakuna maendeleo. Katika jamii tunaona wazi kuwa jamii nyingi
zimeelimika na kupata elimu, japokuwa elimu ambayo tunayo hatuitumii ipasavyo
ili kuleta maendeleo mfano katika kuunda katiba mpya elimu ya hali ya juu
inahitajika ili kujenga misingi ambayo taifa litaitumia katika kuleta maendeleo
na kuondoa umasikini, unyonyaji na hata rushwa ambayo ni adui wa maendeleo.
Hivyo basi ni vyema tukatumie elimu ambazo tumezipata katika maisha yetu kwa
ujumla kwa kufanya hivyo tutakuwa na maendeleo ya hali ya juu.
Wizi
Ni kitendo cha kuchukua mali ya mtu mwingine kwa siri na
kujimilikishia. Katika riwaya hii suala la wizi linaonekana pale ambapo
RIWAYA ZINAZOFANANA NA RIWAYA HII KIMAUDHUI:
Hii riwaya inafanana na riwaya nyingine kama vile;
Ø Simu Ya Kifo (EALB 1965), iliyoandikwa na Katalambula
Ø Kisima Cha Giningi (Evans 1968),
iliyhoandikwa na Mohamed Said Abdulla
Ø Duniani Kuna Watu (EAPH 1973),
iliyhoandikwa na Mohamed Said Abdulla
Ø Siri Ya Sifuri (EAPH 1974), iliyhoandikwa na
Mohamed Said Abdulla
Ø Mwana Wa Yugi Hulewa (EAPH 1976),
iliyhoandikwa na Mohamed Said Abdulla
Ø Kijacho Chembamba (Tamasha 1980),
ilyoandikwa na Ganzel, E
Ø Dimbwila Damu (AP 1984),
iliyoandikwa na Ben Mtobwa
Ø Kosa la Bwana Msa (AP 1984),
iliyhoandikwa na Mohamed Said Abdulla
Ø Mauaji Ni Nani (Jomssi 1987), iliyoandikwa na Simbamwene
Ambazo huzungumzia kuhusiana na
upelelezi (Mlokozi, 1996).
HITMISHO.
Kwa ujumla riwaya hii huzungumzia masuala ambayo
yanajitokeza katika jamii. Mambo haya yanadumu kwa vipindi tofauti tofauti,
kutoka kipindi cha uhuru mpaka leo hii masuala ya umasikini, uchoyo, uzembe
kazini, wizi, rushwa, dhuluma, suala la ukosefu wa upendo wa dhati katika ndoa
na mambo mengine kama vile fitina yamekuwa yakiikumba jamii na kusababisha kurudisha
maendeleo nyuma, hivyo basi ni bora jamii ikaelimishwa na kuachana na haya
masuala kwani yanapoendelea amani inakosekana na kusababisha kukosekana kwa
umoja miongoni mwa wana jamii na kufaya taifa au wanajamii kutopiga hatua
katika sauala zsima la maendeleo.
MAREJELEO
Senkoro F.E.M.K (1987). Fasihi na Jamii: Press and Publicity Center, Dar es salaam.
Senkoro F.E.M.K (2011). Fasihi: Kampuni ya Utamaduni, Tafsiri &Uchapishaji, KATTU,
Dar es salaam.
Muhammed Said Abdulla (2008). Mzimu wa Watu wa Kale: Kenya Literature Bureau, Nairobi.
Mlokozi, M.M (1996). Fasihi ya Kiswahili, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania: TUKI, Dar es salaam.