VIPENGELE VYA KIFANI KATIKA RIWAYA
SWALI: Jadili kipengele cha fani katika riwaya ya
Bina-Adamu kwa kuzingatia mielekeo chomozi ya kifani katika riwaya ya Kiswahili
ambayo ni:
Mwendo wa riwaya.
Naratolojia.
Msuko wa vitushi.
Uhusika na wahusika.
Mtagusano.
Kipengele cha lugha.
Mbinu za kibunilizi.
Mtindo.
YALIYOMO
UTANGULIZI…………………………………………………………………………….…..1
v Historia
fupi ya mwandishi wa riwaya hii ya Bina-Adamu. ……………...……1
v Baadhi
ya kazi zake alizowahi kuandika……………………………………....1
v Muhtasari
wa riwaya hii……………………………………………………..…1
v Uainishaji
wa riwaya hii kwa kujigeza katika kigezo cha fani………………….2
KIINI
CHA KAZI……………………………………………………………………...……....2
v Mielekeo
chomozi ya fani katika riwaya hii……………………………………2
Ø Naratolojia………………………………………………...…………….2
Ø Msuko
wa vitushi…………………………………………...…………..3
Ø Mwendo
wa riwaya………………………………………...…………...6
Ø Mtindo……………………………………………………...…………...7
Ø Uhusika
na wahusika……………………………………...…………….9
Ø Mianzo
na miisho ya riwaya .………………………………………….10
Ø Mtagusano……………………………………………….…………….11
Ø Kipengele
cha lugha…………………………………….……………..12
Ø Mbinu
za ubunilizi……………………………………….…………….15
§ Taharuki...…………………………………….……………...15
§ Utomeleaji…………………………………….……………...16
§ Ujadi………………………………………………….………17
§ Ufumbaji……………………………………………..……….17
§ Dayolojia………………………………………….….……...18
§ Usawili
wa wahusika…………………………………..……..19
§ Ulinganuzi
na usambamba………………………...………….20
§ Mbinu
ya majazi…………………………………..………….20
HITIMISHO………………………………………………………………….………………21
MAREJELEO……………………………………………………………………..………….22
Bina-Adamuni
riwaya iliyoandikwa na Wamitila KyalloWadi na kuchapishwa na Phoenix Publishers
mwaka 2002, Nairobi, Kenya.
Wamitila
KyalloWadializaliwa mwaka 1966 katika nchiya Kenya. Ni mwandishi mwenyeshahada
ya Ph. D katika somo la fasihi. Mwandishi huyuamebobea katika fani za fasihi
ambazo nitamthiliya, hadithi fupi, riwaya na mashairi.Pia ni mhakiki wa fasihi
ambayeamechapishamakala mbalimbali katika majarida ya kisomi Afrika, Ulaya na
Marekani:
Baadhi
ya kazi zake ni kama zifuatazo:
-Bina-Adamu-2002
-Jumba
la Huzuni-2006
-Kamusi
ya Ushairi-2006
-Kuku
na Mwewe-2006
-Harufu
ya Mapera-2012
-Nguvu
ya Sala (Riwaya)
-Shingo
ya MbungenaHadithi Nyingine-2007
-Uncle’s
Jokes-2007
-Wingu
la Kupita
Bina-Adamuni
riwaya inayotumiasitiari ya kijijikuangalia hali ya mataifa ya ulimwengu katika
kipindi hiki ambapo hali za kijamii, kisiasa na kiuchumi zinadhibitiwa na
ubepari wa mataifayaliyoendelea. Hii ni riwaya changamano yenye ufundi wa lugha
na kimtindo, inayomfanya msomaji awaziesiotu yanayozungumzwa bali pia muundo wa
riwaya ya Kiswahili.Hii ni riwaya dhati ambayo ipo katika kigezo cha fani
upande wa riwaya changamano ambazo hutumia lugha fiche, mandhari fiche, majina
na mtiririko wa matukio huwa changamano.
Kwa
mujibu wa Wamitila katika kamusi yake ya fasihi, isimu na nadharia, (2003)
anaonyesha aina tofautitofauti za riwaya kama vile riwaya changamano, riwaya
sahili, riwaya kiambo na nyinginezo. Katika uainishaji huu, riwaya huweza
kuainishwa kwa kutumia vigezo vya kifani, kimaudhui, upeo wa kijiografia na
kigezo cha usimulizi. Pamoja na vigezo vyote hivyo, riwaya huweza kugawanywa
katika makundi makuu mawili yaani riwaya dhati na riwaya pendwa.
Katika
kuainisha riwaya hii ya Bina-Adamu,
tunaiainisha kwa kujigeza katika kigezo cha fani ambapo tunaona kuwa hii ni
riwaya changamani kwa sababu mwandishi ametumia lugha ya mafumbo, hivyo msomaji
anahitajika kuwa na ufahamu wa kutosha ili aweze kuielewa riwaya hii. Kwa mfano
katika ukurasa wa 100, mwandishi anasema:
“Nilikumbuka vituko
kadhaa nilivyopitia huko nyuma kuanzia Zakongwe wazee walinieleza matatizo
mengi waliyokabiliana nayo zamani walipokuwa wakipambana na mazimwi yaliyovamia
nyumba miaka mingi iliyopita.”
Hapa
mwandishi ametumia mazimwi kuelezea jinsi gani nchi za kiafrika zilitawaliwa na
wakoloni na ndipo wakaamua kupambana nao kuwaondoa. Hapa tunaona kuwa ili
msomaji aweze kuelewa maudhui yaliyomo katika riwaya hii anapaswa kutumia
tafakuri ya hali ya juu sana. Mara nyingi waandishi hutumika mbinu hii ya
ufumbaji ili kukwepa mkono wa dola na kuepuka udhibiti wa kazi zao za fasihi.
Mwandishi
wa riwaya hii amefanikiwa kwa kiwango cha juu katika utunzi wake katika
kipengele cha fani na maudhui pia. Kwa kujikita katika kipengele cha fani,
mwandishi amefanikiwa kutumia mielekeo chomozi ya kifani kwa kiasi kikubwa.
Mielekeo chomozi ya kifani ambayo imejidhihirisha katika riwaya hii ni kama
ifuatavyo:
Naratolojia;
hikini kipengele ambacho huelezea namna ambavyo usimulizi umefanyika katika
kazi ya fasihi. Dhana ya usimulizi kwa mujibu wa Madumulla (2009:110), ni dhana
katika fasihi inayobainisha sehemu alipo anayesimulia hadithi au tukio, kwa
jinsi hiyo, msomaji anapata picha ya jinsi matukio yanavyohusiana,
yanavyosababishana na yanavyo endelea mwanzo hadi mwisho.Msimuliaji anaweza
kutumia usimulizi shahidi au usimulizi maizi. Naratolojia husaidia kuelewa
maudhui kutokana na jinsi mtunzi alivyoipangilia kazi yake. Ili usimulizi uweze
kueleweka kwa hadhira, mtunzi hana budi kuwa na taaluma hiyo ya usimulizi na
uzingativu wa lugha anayoitumia kulingana na jamii aliyoikusudia kuifikishia
ujumbe.
Katika kitabu hiki cha riwaya ya Bina-Adamu, usimulizi shahidi umetumika
kwa kiasi kikubwa. Usimulizi shahidi kwa mujibu wa Wamitila (2006:41),ni
usimulizi ambao hutofautiana na usimulizi wa nafsi ya tatu kutokana na sifa
yake ya kutoweza kuyaona yote isipokuwa, kama tulivyoona, usimulizi wa tendi.
Anaendelea kusema kuwa msimulizi anayepatikana katika kazi iliyosimuliwa hivi
huwa ana mkabala mmoja tu maalum. Mawazo anayoyatoa kuhusu tukio mtu au hali
huwa yake tu. Mwandishi wa riwaya hii amejikita kwa kiasi kikubwa katika aina
hii ya usimulizi kwani tunaona matumizi ya nafsi ya kwanza yametumika kwa kiasi
kikubwa sana kuanzia mwanzo wa riwaya hii hadi mwisho japo ametumia aina
nyingine ya usimulizi. Kwa mfano katika ukurasa wa 7 mwandishi anasema:
“Nilipozaliwa
niliwakuta watu wakikiogopa kiini cha kijiji chetu na mpaka leo unapoisoma
hadithi hii bado wanakiogopa.”
Pia
ametumia usimulizi shahidi katika ukurasa wa 32 ambapo anasema:
“Nilishindwa kuelewa. Lakini ili kuuficha
mshangao wangu niliamua kumuuliza maswali.”
Katika ukurasa wa 79 mwandisi anasema:
“Nilianza kujilaumu kwa
kutomwelewa nyanya yangu.”
Pia
usimulizi maizi umetumika kwa kiasi fulani katika riwaya hii. Wamitila
(2006:40) anasema kuwa usimulizi maizi ni usimulizi ambao hufuata mkondo
unaodhihirisha ufahamu wa siri na mambo yote. Katika usimulizi maizi, msimulizi
huwa na sifa za ki-ungu na humaizi na kuelewa kila kitu kinachowahusu wahusika,
mandhari, hadithi, mwelekeo, saikolojia ya viumbe wa hadithini, na kadhalika.
Kwa mfano ukurasa wa 7 mwandishi anasimulia kwa kuwaelezea watu watatu ambao
waliishi kijijini kwao hapo zamani. Mwandishi anasema:
“Mmoja alikuwa mhubiri aliyeishi upande wa
pili unaoelekeana na machweo ya jua. Nyumba yake siku hizi imebakia kuwa banda
kuu baada ya mkewe kuondoka kwa kulalamika chakula kimepotea na wamebakia kula
vyakula vinavyotolewa kama sadaka na waumini.”
Katika
ukurasa wa 8 mwandishi anasema:
“Mkazi wa tatu hakujulikana
kwa jina na watuwengi kijijini. Lakini alikuwa na watoto watatu; huntha
waliondoka zamani na haijulikani walikozamia.”
Msuko
wa vitushi, kwa mujibu wa Mbunda Msokile (1992:206) ni mtiririko au mfuatano wa
matukio yanayo simuliwa kuanzia mwanzo hadi mwisho. Mbinu hii ya Msuko wa
vitushi husaidia katika kufikisha maudhui kwa hadhira na humrahisishia msomaji
katika usomaji.
Pia
Wamitila (2006:6) anatoa maana ya msuko kuwa ni mfuatano wa matukio
yanayopatikana katika kazi ya kifasihi kwa kutegemea uhusiano wake
kiusababishi. Yaani tukio fulani linasababishwa na nini? Hivyo basi kipengele
hiki huangalia motifu mbalimbali alizotumia mwandishi pamoja na mjongeo wa
vitushi.
Motifu
kwa mujibu wa kamusi ya Kiswahili sanifu (2010:963) ni sababu, matilaba au
malengo, msukumo wa kufanya jambo fulani. Zipo aina nyingi za motifu ambazo
zinaweza kutumika katika kazi ya fasihi. Baadhi ya motifu zilizo tumika katika
riwaya hii ni motifu ya safari ambayo huonyesha mhusika au wahusika wakiwa
katika safari.Motifu hii ya safari inajidhihirisha kuanzia sura ya kwanza hadi sura
ya mwisho ya riwaya hii ya Bina-Adamu.
Kwa mfano katika ukurasa wa 12 anasema:
“Nilikuwa bado nimesimama niliposhituka
nimepigwa teke la nyuma na kuambiwa haya anza safari yako ya ufumbuzi.”
Pia
motifu hii ya safari imejidhihirisha katika ukurasa wa 27 ambapo mwandishi
anasema:
“Baada ya safari ndefu
tulitokeza sehemu iliyokuwa na miti mingi ajabu”
Vilevile
katika ukurasa wa 76, mwandishi anasema:
“Badala ya kuifuata ile
njia niliyokuwa nimependekezewa na yule kijana, nilishika njia tofauti
iliyoishia baharini.”
Vilevile
katika ukurasa wa 33 mwandishi anasema:
“Baada ya kutembea mita
kama mia moja hivi, nilitokea mahali palipokuwa na majengo yaliyoonekana kama
ya miaka mingi.”
Pia
ukurasa wa 89, mwandishi anasema:
“Nilianaza safari yangu
tena. Nilikuwa sijaenda mbali niliposikia mmoja wao akiniita kutoka nyuma.”
Motifu
ya safari imejidhihirisha tena katika ukurasa wa 88 ambapo mwandishi anasema:
“Wewe ni Msafiri,”
aliniambia, inamaana bado hujaimaliza safari yako. Jikaze. Ufikapo mwisho wake
utajua maana ya wimbo huu.”
Aina
nyingine ya motifu ambayo imejitokeza katika riwaya hii ni motifu za majini au
baharini. Aina hii ya motifu huhusisha safari ndani ya maji. Katika ukurasa wa
15 mwandishi anasema:
“Niliamua kuufuata
ushauri wake. Hatukuenda sana kabla ya kutumbukia kwenye mto uliokuwa na maji
mengi ajabu lakini hatukuzama, badala yake tulielea juu juu……….”
Pia
katika ukurasa wa 21, mwandishi anasema:
“Nilipozinduka nilikuwa kwenye mto wa ajabu. Maji
yake yalikuwa yakienda kwa kasi ya ajabulakini mara hii hayakuwa yakienda
nyumanyuma bali yalienda mbele”.
Vilevile
mwandishi wa riwaya hii ya Bina-Adamu
ametumia motifu ya mambo ya ajabu ajabu, majini na mazimwi kwa kiasi kikubwa
sana. Motifu hii hujumuisha vitu ambavyo havionekani katika mazingira halisi
lakini huwasilisha dhana fulani kwa hadhira, ambayo ikiletwa katika uhalisia
inaeleweka. Motifu hii imejitokeza sehemu nyingi katika riwaya hii. Kwa mfano
katika ukurasa wa 10, mwandishi anasema:
“Nilijaribu kushikashika hapa na pale kama mtu
asiyekuwa na uwezo wa kuona. Nilishitukia nimepigwa kofi kali “huyu ni nani
anayewakanyaga wanangu? Mjinga gani? Mnatufuatia nini mpaka huku nyie? Wajinga
wakubwa, kwanini hamtosheki na dunia yenu?” ilisema sauti ya kike kwa uchungu.”
Pia
katika ukurasa wa 78, mwandishi anasema:
“Nilipozinduka lile gogo lilikuwa karibu sana
na nilipokuwa nimelala. Nilipigwa na butwaa kubwa. Nililiangalia tena.
Lilichukua sura ya nyanya kisha baada ya muda nikaona likichukua sura ya mke
wangu halafu Hanna.”
Vilevile
mwandishi ametumia motifu hii katika ukurasa wa 14 ambapo anasema:
“Nilipotua nilishitukia
nimesimama na jitu refu, nilijitahidi kusimama ili niweze kuliona jitu hilo
vizuri. Ilikuwa shida kuliona sawasawa. Miguu yake ilikuwa mikubwa ajabu.
Nilirudi nyuma kuweza kuliona vizuri lakini likarefuka nikashindwa kuliona
vizuri.”
Pia
mwandishi anaendelea kuonyesha motifu hii katika ukurasa wa 137, ambapo
anasema:
“Niliguswa bega la
kulia na kugeuka kwa wepesi wa ajabu lakini sikumwona yeyote. Niliangalia mbele
kisha nikaguswa bega la kushoto,usishangae, sauti hapa zinaingiliana, ndio
uhalisia mpya huu.”
Pia
katika Ukurasa wa 156, mwandishi anasema:
“Majini ya pale
yamemshika! Jinsia yake itabadilika!”
Vilevile
katika ukurasa wa 144, mwandishi anaonyesha motifu hii kwa kusema:
“Nilikuwa na nia ya kusogea karibu na kuangalia
vizuri nilipopigwa ngoto kali na kuambiwa kwa sauti ya juu, huna muda wa
kumangamanga hapa kama mmanga. Huntha umewaona au hata kuwatambua? Je, na Peter
P….?”
Aina
nyingine ya motifu ni motifu ya ndoto. Motifu ya ndoto hutumiwa na msanii wa
kazi ya fasihi kwa lengo la kuwasilisha dhamira nzito katika jamii au hutumika
motifu hii kwakukwepa mkono wa dola katika kuwasilishakatikakile alichokusudia
kwa jamii. Wakati mwingine, mwandishi anapotumia ndoto huwa ni mbinu ya kuipa
kazi yake upekee au kuepuka kuwasilisha dhamira kwa njia ya kawaida pasipo
kuonyesha athari ya mhusika moja kwa moja. Katika kuthibitisha hili, mwandishi
anaonyesha ukurasa wa 77 ambapo anasema:
“Ghafla nilisikia sauti
iliyofanana na iliyonijia katika ndoto.”
Kwa
upande wa mjongeo wa vitushi katika riwaya hii ni sahili kwa sababu visa na
matukio yamepangiliwa moja kwa moja kuanzia mwanzo hadi mwisho. Tunaona kuwa
mwandishi anamuonyesha Bina-Adamu jinsi anavyoanza safari yake, vikwazo
anavyokutana navyo katika safari yake hadi anapofika mwisho wa safari yake.
Mbinu hii humsaidia katika kuumba matukio na kuyaendeleza katika kazi za
fasihi,
Mwendo
wa riwaya ni ule mtiririko na mshindilio wa vitushi katika riwaya kwa
kuzingatia vigezo vya Msuko, mandhari, masafa ya kiwakati na kijiografia.
Katika riwaya hii ya Bina-Adamu,
mwandishi ametumia Mwendo wa polepole. Tumebaini kuwa ni Mwendo wa polepole kwa sababu zifuatazo:
Kwanza
mwandishi anasimulia kila tukio hatua kwa hatua ambapo harushi matukio ya
riwaya hii. Usimulizi shahidi uliotumika katika riwaya hii unadhihirisha hili
kwani kila kile anachokisimulia, amekishuhudia. Kwa mfano katika ukurasa wa 54,
mwandishi anasema:
“Nilitokeza mbele ya
wazee waliokaa na vijana kwenye kikundi. Wote walikuwa wakifanya kazi huku
wakiongea. Waliponiona walinijia na kunialika kujiunga nao. Wawili waliondoka
na kurudi na sahani lililokuwa na chakula. Niliwaangalia.”
Pili,
maudhui yaliyotumika katika riwaya hii, kwa kiasi kikubwa ni ya kitanzia kitu
ambacho kinatudhihirishia kuwa Mwendo wa riwaya hii ni wa polepole. Kwa mfano,
katika ukurasa wa 144-145 mwandishi anasema:
“Nakumbuka kijijini
kulikuwa na barabara iliyokuwa na daraja dhaifu. Mwaka mmoja palitumbukia gari
dogo wakafa watu wawili. Viongozi walisema watafikiria la kufanya. Kimya. Miaka
miwili baadaye hali hiyo ikajirudia, mara hii wakasema tumejifunza. Kimya. Mara
ya tatu lilitumbukia basi la abiria wakafa watu mia, ikawa mara hii lazima
tutajenga daraja upya kuzuia tanzia ya kitaifa kama hii. Mpaka leo bado,
wanangojea kukumbushwa.”
Pia
katika ukurasa wa 133, mwandishi anasema:
“Mwenzetu amepigwa
risasi nyingi ajabu, kwa kudhaniwa mwizi, kudhaniwa tu unasikia?”Utanzia
mwingine unaojitokeza katika ukurasa wa 137 na ukurasa wa 148.
Tatu,
Mwendo wa riwaya hii ni wa polepole kwa sababu za kijiografia ambapo mwandishi anaonyesha
mandharia ya kiafrika na mandhari ya kimagharibi kwa kuonyesha kipindi kirefu
ambacho Bina-Adamu alikuwa katika safari yake. Kama mwandishi angeonyesha
maramoja kuwa amefika huko alipokuwa akienda ambako ni nje ya bara la Afrika
pasipo kuonyesha matukio aliyoyafanya njiani, ungekuwa ni mwendo wa haraka.Kwa
mfano katika ukurasa wa 130-131 anaonyesha majengo ya Mefu na jengo la Pembetano
ambako Bina-Adamu alikuwa amefika huko.Pia mwandishi anaonyesha mandhari ya
nchi za kimagharibi katika ukurasa wa 119 anaposema:
“Darling, huyu anatoka
jana. Hawa ndio wanaojua furaha. Nilitamani kuwaeleza kuwa maisha yetu yalikosa
furaha kwa sababu ya umasikini na uongozi mbaya.”
Katika
maneno hayo hapo juu, ni ya watu wawili ambapo awalimmoja alikuwa Afrika lakini
kwa wakati huualikuwa nje ya Afrika na kukutana na mwenzake huko ughaibuni.
Mwendo
wa riwaya husaidia katika kubaini masafa ya wakati na masafa kijiografia katika
kazi za fasihi.
Mtindo
kwa mujibu wa Wamitila (2006: 28),ni upangaji wa fani na maudhui katika kazi ya
fasihi kwa njia ambayo hatimaye hutokeza au huonyesha nafsi na au labda upekee
wamtunzi huyu. Kwa ujumla, mtindo hurejelea mbinu aitumiayo msanii wa kazi ya
fasihi katika kufikisha ujumbe wake.Mwandishi wa riwaya ya Bina-Adamu ametumia monolojia kwa kiasi kikubwa katika kazi yake
kwanzia sura ya kwanza hadi sura ya mwisho. Katika ukurasa wa 7, mwandishi
anasema kuwa:
“Nilipozaliwa
niliwakuta watu wakikiogopa kiini cha kijij chetu na mpaka leo hii unapoisoma
hadithi hii bado wanakiogopa. Kijiji chenyewe kimezungukwa na mito isiyokaukwa
na maji pande zote na kimejitenga na vijiji vingine vinavyohusiana nacho kama
Utaridi na Kausi. Katikati pana mti mkubwa ulioota na unaoonekana na mtu akiwa
mbali na kilipo kijiji chenyewe”.
Pia
ametumia dayolojia ili kuipa uhai kazi yake. Katika ukurasa wa 15,mazungumzo
kati ya Hanna na Bina-Adamu mwandishi anasema:
“Mimi naitwa Hanna,
unaweza ukasema Anna ukitaka’’,aliniambia. Anaongea kama yeye kabisa,
nilijiambia.”
“Hapa ni wapi?”
“Umeuliza swali hilo mapema mno! Ulipotoka
hukufunzwaharakaharaka hainaBaraka?”
Hayo
ni mazungumzo kati ya Bina-Adamu na Hanna,alipokuwa nataka kujua ni wapi aliko
na anaelekea wapi. Majibizano pia yametokea uk 34-35, piauk. 47 mazungumzo
baina ya Bina-Adamu na mzee mmoja aliyekuwa anamwambia Bana-Adamu asimshangae:
“Usishangae Bina-Adamu Msafiri!” alisema Yule
mzee kwa sauti dhaifu lakini imara.
“Kulifanyika nini huku?” niliuliza.
“Matokeo ya mchezo!”
“Wa nani?...…..”
Majibizano
pia yametokea uk 68-69,uk 70-71, uk 95-97,uk 108,uk 119,uk 124,uk 127-128,uk
130,uk 141-142,uk147,uk 150-151,uk 152-153,uk 154-156.
Matumizi
ya nafsi katika riwaya hii yaBina-Adamunafsi zote
tatu zimetumika lakini nafsi ya
kwanza na ya tatu ndizo zilizotumika kwa
kiasi kikubwa zaidi kuliko nafsi ya pili.
Kwa kuanza na nafsi ya kwanza umoja
hii ndiyo imetawala kwa kiasi kikubwa
takribani riwaya yote kwa mfano
nafsi ya kwanza umoja
imetumika ukurasa wa 7 mwandishi anasema:
“Nilipozaliwa
niliwakuta watu wakikiogopa kiini cha kijiji chetu na mpaka leo hii unapoisoma
hadithi hii bado wanakiogopa”
Pia matumizi ya nafsi ya kwanza
yanajitokeza katika ukurasa wa 11, 12, 15, 27, 52, 59, 67.87, 119, 121, 129 na
kadhalika.
Vilevile nafsi yakwanza wingi imeonekana
katika ukurasa wa 74 mtunzi anasema:
“Tulizunguka kuangalia nyumbanyingine
lakinitukashindwa kuzimaliza kwa siku moja”
Matumizi yanafsi ya pili umoja na uwingi
pia yamejitokeza kwa kiasi kidogo. Mfano nafsi ya pili umoja katika ukurasa wa 16, 88, 124,125 na 154 na
nafsi ya pili uwingi
inajidhihirisha katika ukurasa wa 112
mwandishi anasema:
“Tatizo
lenu kuu, hamtaki kuukabili uhalisia wenu na kujitahidi kuubadilisha……………”
Pia kwa kiasi fulani nafsi ya tatu
imetumika katika umoja na uwingi .kwa
kuanza na nafsi ya tatu
umoja nafsi hii
imetumika katika kurasa zifuatazo 18, 19, 50,
55, 58, 86,
87, 97, 103, 108, 117, 124,
126, 128, 132, na sehemu nyinginezo. Mfano katika ukurasa wa 132 mtunzi
anasema:
“ Alinizungusha nyumbani
akinieleza , “ Hii ni friji
ambayo ina uwezo wa kumfanyia
mtu mambo mengi.”
Kwa upande wa nafsi ya tatu uwingi imejitokeza katika ukurasa wa
17, 19, 38, 50, 57, 99, 100, 101, 102, 113 na kadhalika. Mfano katika ukurasa
wa 100 mwandishi anasema:
“Walielezea matatizo waliyoyapata siku hizi: karo
ya watoto, upungufu wa chakula, magonjwa, matatizo ya kazi, hospitali kukosa
dawa, wizi wa nguvu; tuseme shida za kila aina.”
Pia katika kipengele cha mtindo,
mwandishi hutumika lugha kwa namna ya kipekee sana na kibunifu sana. Kipengele
cha matumizi lugha kitajadiliwa kwa undani katika mbinu za kibunilizi na katika
mtagusano ambapo kuna matumizi ya lugha mbalimbali.
Umuhimu wa matumizi
ya nafsi ya kwanza ni kuonesha ushahidi wa matukio anayoyasimulia kwa hadhira
yake kwa ukina. Na matumizi ya nafsi ya
pili humufanya msomaji kujiona kuwa yeye ndiye mlengwa mkuu wa kazi husika.
Matumizi ya nafsi ya tatu humweka karibu msomaji wa kazi husika.Mbinu hii ya
mtindo, hutumika kwa lengo la kuipa uhai kazi ya fasihi, kuwachora wahusika
wake, kuonyesha upekee wa kazi ya mtunzi na kufikisha ujumbe kwa hadhira.
Uhusika na
wahusika. Wahusika kwa mujibu wa Senkoro, (2011:7) ni watu ama viumbe
waliokusudiwa wawakilishe dhana, mawazo au tabia za watu katika kazi ya fasihi.
Uhusika wa wahusika katika riwaya ya Bina-Adamu
unajitokeza pale wanapopewa sifa na tabia fulani na kuweza kuwa wawakilishi wa
watu wema au wabaya. Katika riwaya hii
mwandishi ameonyesha wahusika wanaojipambanuawaziwazi na wahusika ambao
hawajipambanui waziwazi.
Wahusika
ambao wanajipambanua waziwazi ni kama vile, Mhubiri, Mwanasayansi, Kichaa na
Bina-Adamu Msafiri. Kila mhusika, uhusika wake unaonekana katika riwaya hii
kulingana na mwandishi wa riwaya hii alivyompa uhusika huo. Kwa mfano uhusika
wa Bina-Adamu unajidhihirisha kuanzia
mwanzo wa riwaya hii hadi mwisho. Uhusika wake unaonyesha matendo na tabia
ambazo zinastahili kuigwa katika jamii kwani anaonyesha juhudi ya kufanya
uvumbuzi ambao unaibua dhamira ya upelelezi na kufanya mapinduzi.
Pia
mwandishi ameonyesha wahusika ambao hawastahili kuigwa katika jamii kutokana na
jinsi walivyochorwa na mwandishi. Kwa mfano P.P ambaye ni Peter Pan hastahili
kuigwa katika jamii kwa mfano, Ukurasa wa 71 mwandishi anasema:
“Sasa huyu P.P ni nani
anayeelekea kuhusika na kila kitu? Nilijiuliza. Niliyakumbuka maafa niliyoyaona
huko nyuma nilikoelezwa yalitokana na bomu lake.”
Pia
mwandishi ametumia wahusika ambao uhusika wao ni wa ajabuajabu kwa sababu wana
sifa kama mizimu. Kwa mfano. Mwanishi anamchora mhusika Hanna kama mhusika
ambaye anabadilikabadilika na wakati mwingine anatokea na kupotea. Mwandishi
anathibitisha hili katika ukurasa wa 32 kwa kusema:
“Hanna alikuwa
ametoweka sasa lakini wale viumbe wa ajabu walikuwa wakiongoza njia,”
Licha
ya mwandishi kutumia wahusika wanaobadilikabadilika wamefanikiwa kuonyesha
uhusika wao kwa kutoa msaada mkubwa wa kumwongoza Bina-Adamu.
Kwa upande wa wahusika wasiojipambanua
waziwazi, mwandishi anamwonyesha mhusika X katika ukurasa wa117 ambapo
mwandishi anasema:
“Jina langu ni X. Basi
karibu leo na kesho. Karibu utafika kwenye Bustani ya Eden ya pili!”
Mianzo
na miishoni mbinu ambayo hutumiwa na wasanii wa kazi za fasihi katika kazi zao
kwa kusudi la kuiandaa hadhira katika kazi husika, kuonyesha mwazo wa hadithi
na uhitimishwaji wa hadithi. Mbinu hii mara nyingi hutumika katika kazi za
fasihi simulizi na katika fasihi andishi kwa kiasi kidogo. Kazi za kifasihi za
zamani zinautofauti mkubwa sana kwa na kazi za siku hizi. Kazi nyingi za
kifasihi za zamani zilikuwa zikifuata mianzo na miisho ya kifomula kwa sehemu
kubwa tofauti na kazi za siku hizi ambazo mara zinakuwa na mianzo ya kawaida.
Mwandishi wa riwaya hii ya Bina-Adamu
ametumia mianzo ya kawaida ambayo siyo ya kifomula. Kwa mfano katika ukurasa wa
7, anaanza kwa kusimulia visa vyake moja kwa moja pasipo kufuata mianzo ya
kifomula ambavyo huanza kwa namna ya kipekee kama vile, “hadithi hadithi…..”,
“puakwa…..pakawa”, na mianzo mingineyo. Mwandishi anaanza kwakusema:
“Nilipozaliwa
niliwakuta watu wakiogopa kiini cha kijiji chetu na mpaka leo unapoisoma
hadithi hii bado wanakiogopa. Kijiji chenyewe kimezungukwa na mito isiyokaukwa
na maji pande zote.”
Pia
katika kuhitimisha riwaya hii, mwandishi hajaonyesha miisho ya kifomula ambayo
mara nyingi huishia na maneno kama vile, “hadithi yangu ikaishia hapo”, na
“wakaishi kwa raha mstarehe”. Mwandishi amemalizia kazi yake kwa kawaida sana
ambapo anaiacha hadhira yake bila kuridhika kwani haonyeshi dhahiri nini
kiliendelea baada ya Bina-Adamu kufika alipokuwa amekwenda kuwatafuta huntha
watatu jambo ambalo ni tofauti na kazi nyingi za kifasihi ambazo huwa na miisho
ya kifomula.
Mtagusano
ni kipengele kinachohusiana na muingiliano wa vipengele mbalimbali katika kazi
ya fasihi kutokana na athari za utamaduni na sayansi na teknolojia. Mtagusano
umejitokeza kama dhamira, madhari na lugha.
Mtagusano
unajidhihirisha katika riwaya hiikwa kusadifu dhamira za kimagharibi kama vile
uonevu ambapo waafrika wanateswa na kuonewa pindi waendapo nchi za magharibi.
Kwa mfano katika ukurasa wa 133, mwandishi anasema:
“Mwenzetu amepigwa
risasi nyingi ajabu kwa kudhaniwa mwizi; kudhaniwa tu, unasikia? Tunajua tu ni
kwa sababu ya rangi tu, unasikia rangi tu!”
Pia
mtagusano kama dhamira, unajidhihirisha katika ukurasa wa 128 ambapo tunaona
watu wakiufanyia uchunguzi ubongo wa Alberty Einstean ili kuweza kutambua akili
alizokuwa nazo kabla ya kifo chake. Mwandishi anaonyesha dhamira hii ambayo
inafungamana na dhamira za kimagharibi wa kuonyesha namna watu wenye upeo
mkubwa wa akili wanavyofanyiwa katika nchi zilizo endelea. Mwandishi anasema:
“Kwanini Albert
Einstein alikuwa na akili za ajabu. Tunauchunguza ubongo wake sasa!”
“Ubongo wake?”
“Ehh, tuliufukua baada
ya kifo chake!”
“Huku hakuna miiko?”
“Baada ya kifo
aliipoteza haki ya mwili wake. Tunachunguza kiini ili kuiendeleza jamii ya
kesho.”
Kwa
upande wa mandhari kama mtagusano, mwandishi anatumia madhari ya kimagharibi
kwa sehemu kubwa na hivyo kutumika kama mtagusao. Mwandishi anathibitisha hili
kwa kusema:
“Kwanza kuna jengo la
Mefu” (ukurasa wa 130)
“Jengo la pili ni
Pembetano” (ukurasa wa 131)
Pia mwandishi ametumia lugha za kigeni katika
kazi hii. Kwa mfano katika ukurasa wa 20 ametumia neno la kilatini Vitas lenye maana ya maisha. Pia ukurasa
wa 38 ametumia neno la kijerumani Fyuraa
ambalo kwa Kiswahili linamaanisha kiongozi. Vilevile mwandishi ametumia maneno
ya kiingereza kwa kiasi kikubwa. Kwa mfano; International
water (ukurasa wa 50), Reconditioned
car (ukurasa wa 50), Global village
(ukurasa wa 87), Global pillage
(ukurasa wa 87), Darling (ukurasa wa
119), the soul of Black folk, (ukurasa wa 126), Balance of power (ukurasa wa 142), Dollar (ukurasa wa 142), Rhythm (ukurasa wa 143), na Global villain (ukurasa wa 155).
Matumizi
ya lugha, mwandishi ametumia lugha nyepesi na ya kawaida iliyojaa Methali,
nahau, vitendawili, tamathali za semi na mbinu nyingine ya kisanaa ili
kufikisha ujumbe kwa hadhira kwa mujibu wa Senkoro (2011) fasihi ni sanaa itowayo
maudhui yake kwa kutumia lugha ya maneno ambayo hutamkwa ama kuandikwa.
Kipengele hiki ni muhimu sana kwani ndicho kinachotofautisha fasihi na sanaa
nyingine. Kwa kiasi kikubwa mwandishi wa riwaya hii ametumia lugha ya kawaida
iliyojaa misemo, methali, tamathali za sina mbinu nyingine za kisanaa kama
ifuatayo.
Misemo
na nahau, katika riwaya hii misemo na nahau vimeonekana katika kurasa mbalimbali
kwa lengo la kuijulisha hadhira wakati unaohusika katika kazi ya fasihi husika,
misemo hiyo imesawiriwa na mwandishi kama ifuatavyo:
Usiwe yule fisi wa
masimulizi (uk.54)
Kichwa
cha nyoka hakistahimili kilemba (uk13)
Msahau
jana kesho humkumbusha (uk125)
Kila
ukombozi unahitaji shujaa (uk128)
Usipende
mwanga kabla hujalijua giza (uk106)
Kuaga
dunia (uk47)
Methali,
hizi ni semi fupi fupi zenye kueleza kwa muhtasari fikra au mafunzo mazito
yaliyotokana na uzoefu wa jamii (Mlokozi 1989). Katika riwaya hii mtunzi
ametumia methali mbalimbali kamavile;
“Msahau jana kesho
humkumbusha” (uk.125)
“Mgeni njoo mwenyeji
apone” (uk.139)
“Haraka haraka haina
Baraka” (uk.23)
“Kidole kimoja
hakivunji chawa” (uk.88)
“Hasira hasara”
(uk.15)
“Mwenye pupa hadiliki
kula tamu” (uk.140).
“Kigumba
kwa nguruwe kwa binadamu kichungu” (uk143)
“Kichwa
cha nyoka hakistahimili kilemba” (uk13)
“Msahau
jana kesho humkumbusha” (uk125)
“Kila ukombozi
unahitaji shujaa” (uk128)
“Usipende
mwanga kabla hujalijua giza” (uk106).
Mwandishi
katumia methali, misemo, vitendawili na nahau kwa lengo la kumfanya msomaji asichoke,kuonyesha
ufundi wake katika lugha anayoitumia, kuweka msisitizo juu ya jambo fulani, pia
matumizi ya misemo kama methali husaidia kuonya jamii juu ya jambo fulani.
Tamathali
za semi ni maneno au sentensi ambazo hutumiwa na wasanii wa fasihi ili kuvitia
nguvu katika maana, mtindo na hata sauti katika maandishi ama kusema. Katika
riwaya hii mwandishi ametumia tamathali za semi mbalimbali kama zilivyoainishwa
hapo chini.
Tashibiha,
hii ni hali ya kulinganisha vitu viwili au zaidi kwa kutumia maneno kama vile; “kama”,
“mithili” na “mfano wa”. (Senkoro 2011).
Tamathali
hii imetumika katika riwaya ya Bina Adam!
Mfano:
“Umati wenyewe umekodoa
macho pima huko juu kama kuku anayemwangalia mwewe”
(uk.69)
“Nilivuta tabasamu na
kutoa pumzi kama kiboko kasha nikaogelea hadi ukingoni na kutoka” (uk.77)
“Lakini niliweza
kuziona pia zake za miguu zilizokuwa kubwa kama masahani” (uk.63)
“Anaendelea
kung’ang’ania mlingotini tu kama kima”(uk.91)
Tashihisi,
hii ni tamathali ambayo vitu visivyokuwa na sifa za binadamu hupewa sifa za
kutenda kama binadamu. Mfano katika riwaya hii tamathali hii imejitokeza kama
ifuatavyo,
“Uwongo umechukua kiti
na kuketi kijijini”(uk.75)
“Huko mbele kulikuwa na
msululu mkubwa wa milima”(uk.32)
“Niliamua kuifuata ile
njia pana iliyoishia kunitokomeza”(uk.144)
Mbinu
nyingine ya lugha iliyojitokeza katika riwaya hii ya Bina-Adamu ni:
Tanakali
sauti, haya ni maneno yaundwayo kutokana na sauti zinazofanana nayo. Mfano
katika (uk.125) mwandishi ameandika:
“Kutokwa na machozi
yaliyoanguka nde! Nde! Nde!”
Mdokezo,
hii ni hali ya kutamka maneno bila kuyamalizia ili kuleta maana halisi. Mfano
katika (uk.122)
Mwandishi
ameandika:
“Hi..i.ndiyo...njia…a a
ya..peke..e..e. kuhakiki..isha kuwa hukw..amizwi…pia katika”
(uk.21)
Pia
mwandishi ameandika:
“Nyoka…Nyoka…..”
Takiriri, hii ni
tamathali ya semi ambapo sehemu ya neno hurudiwa rudiwa au neno zima. Mwandishi
hutumia mbinu hii kwa ajili ya kusisitiza juu ya jambo fulani. Katika riwaya
hii mwandishi ametumia takriri kuonyesha msisitizo wa mambo anayoyazungumzia
katika kazi yake, takriri zilizo tiumika ni kama vile:
“Beberu
…….!Beberu……!Beberu……….!Nilijiambia akilini nikiliangalia, beberu, beberu,
beberu, linanuka beberu” (uk14)
“Kwanini?
Kwanini? Kwanini?” (uk 22)
“Hatimaye
nilianza kutapika. Nikatapika, nikatapika, nikatapika”. (uk83)
“Nyoka …….! Nyoka………!”
(uk21)
Pia
riwaya hii imeshehenezwa na taswira kwa kiasi kikubwa. Madumulla J. S (2009:
153) akimnukuu Senkoro F. M. E. K,anasema,taswira ni mkusanyiko wa picha mbali
mbali ziundwazo kwa maelezo ya wasanii katika kazi ya fasihi. Anaendelea kusema
kuwa ni lugha inayochora picha ya vitu au mahali kwa kutumia ishara.
Hivyo,
taswira ni lugha ya picha ambayo hutumiwa na mtunzi kufikisha ujumbe mzito kwa
hadhira. kuna aina mbili ya taswira yaani ya wazi ambayo huwa na mkusanyiko wa
picha mbali mbali zinazotoa ujumbe wa moja kwa moja bila kuficha na zisizowazi
ni zile ambazo hazitoi ujumbe wa moja kwa moja ambayo humhitaji msomaji afikiri
sana.
Katika
riwaya ya Bina-Adamu mwandishi
ametumia taswira mbali mbali katika kufikisha ujumbe, taswira hizo ni kama
zifuatazo:
“Kijiji”- mataifa ya ulimwengu katika kipindi hiki
hali za kijamii, kisiaa na kiuchumi zinadhibitiwa na ubepari wa mataifa
yaliyoendelea (juu ya jarada)
“Paani”- madarakani (uk. 67)
“Maganda, makokwa na makaka”- kile kidogo wanacho
kipata watu
“Ngazi”-dhamana ya kuingia madarakani
“Matunda”-utajiri.
“Kitambara”-bendera (uk. 68)
Taswira zingine ni mawe, beberu, mkoba na nyingine
nyingi.
Umuhimu wa kutumia mbinu hiii, ni kukwepa mkono wa
dora, kufikisha ujumbe kwa hadhira na kumfakarisha msomaji wa kazi ya fasihi.
Kipengele
kingine cha mwelekeo chomozi wa kifani uliotumika katika riwaya hii ya Bina-Adamu ni mbinu za kibunilizi.Mbinu
za kibunilizi ni mbinu mbalimbali za kiubunifu ambazo huzipa kazi za fasihi
upekee. Mbinu hizi za kibunilizi ambazo zimejitokeza katika riwaya hii ni kama
zifuatazo:
Taharuki
kwa mujibu wa Wamitila (2006:8) ni ile hali ya matarajio ambapo tuna hamu ya
kutaka kujua kitakachotokea baadaye. Anaendelea kusema kuwa ni hali ya
kusisimua inayompata na kumshika msomaji kiasi cha kuwa na hamu kubwa ya kujua
hali au mambo ya baadaye. Pia Senkoro (2011:70) anasema kuwa ujengaji
wataharuki hutofautiana kutoka mtambaji mmoja na mwingine, hata kama kisa
kinachoelezwa ni kilekile kimoja. Katika riwaya hii mwandishi amefanikiwa kwa
kiasi kikubwa kwa kuijenga kazi yake kitaharuki toka mwanzo wa riwaya hadi
mwisho. Msomaji anakuwa na hamu ya kutaka kujua nini kitakachotokea katika
safari ya Bina-Adamu Msafiri katika harakati za kuwatafuta Huntha watatu.
Katika riwaya hii msomaji anataka kujua uvumbuzi utakaofanywa na Bina-Adamu.
Kwa
mfano katika ukurasa wa1mwandishi anasema:
“Nilipozaliwa niliwakuta watu wakiogopa kiini
cha kijiji chetu na mpaka leo hii unapoisoma hadithi hii bado wanakiogopa.”
Hivyo
msomaji hupata dukuduku la kutaka kufahamu juu ya nani Msimuliaji,na ni pahala
gani panaposimuliwa na hivyo kuendelea kusoma kazi hiyo ili afahamu juu ya
simulizi husika. Pia kazi hii inamjengea taharuki msomaji kwa kutaka kung’amua
kuwa P.P ni nani ambaye amechorwa kwa kufumbwa toka mwanzo na jina lake kamili
linakuja kujulikana mwishoni kuwa ni Peter Pan. Kwa mfano uk 151,
“Umesema Peter ..e..e..r?Ndiye
P.P. kumbe?”
“Ndiye huyu!
“Hiyo P ya pili
inamaanisha nini?”
“Jina lake kamili ni
Peter P…”
“Kumbe ndio maana
anatupa mawe ovyo ovyo tu!”
Hivyo,
matumizi ya taharuki humsaidia sana msomaji kupata hamu ya kuendelea
kusoma.Vile vile taharuki humtoa uchovu msomaji na kuinua ari mpya ya kusoma.
Kipengele
kingine cha mbinu za kibunilizi ambacho kimejidhihirisha katika riwaya hii ya Bina-Adamu ni utomeleaji. Huu ni
uchopekaji wa vijitanzu vingine vya fasihi ambavyo ni tofauti na utanzu
unaoshughulikiwa. Riwaya ya Bina-Adamu
imejengwa kwa utomeleaji ndani yake. Hili linajidhihirisha katika ukurasa wa 87
ambapo mwandishi anaonyesha wimbo ufuatao
“Shusha,
shushaa…….thamani ya hela shushaaa!
Bana, banaa….ugavi wa
hela banaa!
Kata, kata…..matumizi
ya hela kataa!
Hurisha, hurishaa……soko
la hela hurishaa!
Punguza,
punguzaa……mishahara duni punguzaa!”
Vilevile
wimbo umejitokeza katika ukurasa wa 149, ambao unasema:
“Oh nchi hii! Nchi
yangu niliyoivumbua……
Enzi yangu, salama
uongozwapo na mfalme mmoja
Chimbuko la johari za
gharama
Oh, jinsi ulivyotukuka
uvumbuzi wako
Kuingia katika duara
hii ni kuwa huru
Suala si KUWA, SWALI NI
WAPI PA KUWA!”
Pia
mwandishi ametumia mbinu ya ujadi. Ujadi ni matumizi ya kauli ambazo
hufungamana na jamii husika iliyokusudiwa na mwandishi. Hii inaonekana pale
mwandishi anapotumia methali, vitendawili na nahau. Baadhi ya methali hizo ni:
“Haraka haraka haina
Baraka” (ukurasa wa 23)
“Hasira hasara”
(ukurasa wa 15)
“Msahau jana, kesho
humkumbusha” (ukurasa wa 125)
“Matumaini ni chajio
kizuri lakini kiamsha kinywa kibaya”
(ukurasa wa 88)
Vitendawili,
katika ukurasa wa 82 ambapo mwandishi anasema:
“Muda si muda
nilishindwa hata kupiga hatua moja kutokana na giza lahuku ng’o na kule ng’o msituni.”
Ufumbaji
ni matumizi ya kauli zenye maana fiche katika kazi za fasihi. Mwandishi
ametumia mbinu ya ufumbaji kwa kiasi kikubwa. Ufumbaji umejitokeza katika
uumbaji wa mandhari, katika lugha, katika maudhui na katika uumbaji wa
wahusika.Katika uumbaji wa mandhari, mwandishi amejitahidi kuyaficha sana. Siyo
rahisi kuyatambua kwa urahisi pasipo kufanya uchunguzi wa kutosha. Aidha
ametumia mandhari ya nchi za kiafrika na yale ya kimagharibi. Kilicho bainisha
hapa na kufanya madhari ya kimagharibi kujulikana ni kutumia maneno kama vile
jengo la pembe tano ambalo linatufanya tubaini kuwa nchi inayozungumziwa ni
Marekani ambako kuna jengo la Mefu na jengo la Pembetano, maarufu kama
Pentagonijapokuwa hajaitaja nchi husika kwa uwazi kama ni nchi ipi. Mwandishi
anayazungumzia majengo haya katika ukurasa wa 130 na 131. Anathibitisha hili
kwa kusema:
“Kwanza kuna jengo la
Mefu” (ukurasa wa 130)
“Jengo la pili ni
Pembetano” (ukurasa wa 131)
Pia
ufumbaji katika mandhari unaojitokeza katika ukurasa wa 133 na 134. Katika
ukurasa wa 133, mwandishi anasema:
“Kumbe hata huku
wanawapiga risasi watu kwa kuwadhani ni wezi? Je, kama huku msingi wao mkuu
ulikuwa rangi, kwetu ulikuwa nini ambako watu wanapigwa risasi na polisi kila
mara?”
Katika
ukurasa huu mwandishi anaendelea kusema:
“Kila siku P.P
anasisitiza hii ndiyo nchi bora katika sayari zote”!
Katika
kipengele cha lugha, ufumbaji umejitokeza katika riwaya hii. Mwandishi ametumia
lugha iliyojaa taswira, misemo, tamathali za semi, misemo na mbinu mbalimbali
katika kipengele hiki jambo ambalo linamfanya msomaji wa riwaya hii kuwa na
tafakuri ya hali wa juu ili aweze kubaini kilichokuwa kimekusudiwa na
mwandishi. Kwa mfano, katika ukurasa wa 100, mwandishi anatumia lugha ya
mafumbo kwa kusema:
“Nilikumbuka vituko
kadhaa nilivyopitia huko nyuma kuanzia Zakongwe wazee walinieleza matatizo
mengi waliyokabiliana nayo zamani walipokuwa wakipambana na mazimwi yaliyovamia
nyumba miaka mingi iliyopita.”
Vilevile
ufumbaji umejitokeza katika uumbaji wa wahusika. Mwandishi ametumia wahusika
fiche na baadhi yao kuwapa sifa ambazo kiuhalisia hawawezi kuwa kama
walivyopewa uhusika wao katika riwaya hii. Kwa mfano ameweza kumchora mhusika
Hanna ambaye ana matendo ya ajabu ajabu ambapo anakuwepo mahali fulani kwa
wakati fulani na kutoweka ghafla wakati mwingine. Katika ukurasa wa 32,
mwandishi anasema:
“Hanna alikuwa ametoweka sasa lakini wale viumbe
wa ajabu walikuwa wakiongoza njia,”
Pia
amemtumia mhusika P.P ambaye hajipambanui wazi wazi na kujulikana kwa wepesi.
Hata Bina-Adamu Msafiri alikuwa na shauku ya kumjua huyu mhusika hadi mwisho wa
riwaya hii. Licha ya jina lake kujulikana mwishoni kama Peter Pan; bado siyo
rahisi kumwelewa mhusika huyu kama alikuwa anawakilisha mtu gani katika
mazingira halisi ya Magharibi.
Mbinu
nyingine ya kibunilizi ni matumizi ya dayolojia. Dayolojia ni mazungumzo ya majibizano
baina ya wahusika wawil au zaidi wanaozungumza kwa kupokezana.Katika riwaya ya Bina-Adamu mwandishi ametumia mbinu hii
ili kuwezesha kuondoa uchovu kwa wasomaji wake.Pia kupitia mbinu hii ya
kibunilizi mwandishi ameweza kujiongezea ufundi wa kiutunzi kwa mfano katika ukurasa
wa 23 kuna majibizano kati ya Hanna na Bina-Adamu,
“Hapa ni wapi?”
“Umeuliza swali hilo
mapema mno! Ulikotoka hukufunzwa haraka haraka haina Baraka”
“Na nani?”
“Na babu!”
“Ala, amemjuaje huyu? Au
labda ni mke wangu katika sura nyingine?”
Vilevile
dayolojia imejitokeza katika uk 34 mwandishi anasema:
“Wewe ndiye Bina-Adamu
msafiri?”
“Ehhh…”
“Tulijua utapita hapa!”
“Mliambiwa na nani?”
“Na babu yako.”
“Babu alikufa miaka
mingi iliyopita!”
“Kumbe? Ndiyo maana
hata kuongea kwake kulikuwa kwa shida!”
Pia
dayolojia imejitokeza katika ukurasa wa 35,47,68,70,71,na72.Tunaona matumizi haya ya dayolojia yanaonesha kila
hatua ambayo mhusika Bina-Adamu msafiri amepitia na vikwazo alivyokutana
navyo.Umuhimu wa matumizi ya dayolojia katika masimulizi ni kumuwezesha msomaji
kufuatilia kila kinachotokea katika riwaya.Vilevile humfanya msomaji asichoke
kusoma kazi husika anayoisoma.
Usawili
wa wahusika ni mbinu nyingine ya kibunilizi ambayo hutumiwa na mtunzi kwa lengo
la kuwachora, kuwaelezea,kuwafafanua na kuwatambulisha kwa kuwapamajina, dhima,
sifa, tabia na matendo. Katika riwaya ya Bina-
Adamu mwandishi ametumia mbinu ya maelezo,ulinganuzinausambamba, kuzungumza
na hadhira, namajazi kwa nia ya kuwachora na kuwafafanua wahusika wake.
Mbinu
ya maelezoniileinayotumia ufundi wa mtunzi katika kuelezea wahusika wake, mbinu
hii imetumiwa katika kitabu hiki cha Bina-
Adamu katika ukurasa wa 7mpaka 8, unasema:
“Zamani za kale
paliishiwakaziwachachesana na labdawatatu. Mmoja alikuwanimhubirialiyeishi
upande wa pili unaoelekeana na machweo ya jua. Nyuma yake siku hizi imebakia
kuwa bandakuubaada ya mkwewekuondokakwakulalamikachakulakimepotea na
wamebakiakulavyakulavinavyotolewa kama sadaka na waumini. Ukiinamia upande wa
pili kulikuwa na kichaaaliyeishi upande huo katika kibandakilichofanana na
kidungu cha kuwingiandegeshambani; kipompakaleo.
Wanakijijiwanasemakichaahuyoalikuwamgangakabla ya
wanakijijikumbatizakichaa.Hadithi yake inasimuliwa kwenye vijiji vya
mbaliwanakoamini kuwa alikufamiakamingiiliyopita. Mkaziwa tatu hakujulikana kwa
jina na watu wengi kijijini. Lakini alikuwanawatotowatatuhuntha;
Waliondokazamani na haijulikaniwalikozamia.”
Kutokana
namaelezo ya mwandishi tunatambua sifa, tabia na matendo ya wahusika hawawatatu,
mbinu hii humfanya mtunzi awe karibu na jamii yake.
Mbinu
nyingine ni kuzungumziwa na wahusika wengine ambapo wahusika waliotumika na
mwandishi wanatoa sifa na tabia za mhusikamwingine. Mbinu hii imejitokeza
katika ukurasa wa 71 unasema:
“Mwalimualiwaeleza ni
kwaninihuyo P. P anawatupia watu mawe kwa kumbwewe?
“Alisemaanapendakuchezachezatu”
“Kuwatia watu vivimbe
vichwani?”
“Tuliambiwa ni mtundu
na jeuri”
“Wa kuwagotoa watu
vichwa?”
“Labdakwake huo ni
mchezo!”
Pia,
imejitokeza katika ukurasa wa 24, 55 na 71
Ulinganuzi
naUsambamba ni mbinu bunilizi ambayo hutumika na mtunzi kwa njia ya
kuwafafanisha na kuwatofautisha kati ya mhusika mmoja au zaidi na wahusika
wengine. Mbinu hii imetumika katika ukurasa wa 67:
“Kila
kiongozi anakaahuko juu paani, hukondikoanakochumiamatundakwaurahisi na
kuwatupia watu walioko chini ambao ndiowaliomshikiangazi ya kupanda juu. Lakini
kamawengine ambao wanachofanya ni kulawakashiba kwanza kasha kuyatupa makaka,
makokwa na maganda huko chini yanakong’aniwa na umati mkubwa ulioko huko.
Wengine wanaibana kuhamishia kwingine, labda ughaibuni”. Katika mbinu hii
tunapata sifa, tabia na matendo ya wahusika kwa kuwatofautisha na wahusika
wengine.
Wamitila
(2006) anasema kuwa, mbinu ya majazi ni mbinu au njia sahali au nyepesi sana ya
uhusika, waandishi wa kazi za kifasihi huweza kuyatumiamajina ya wahusika
ambayo huakisi mandhari, wasifu, tabia,itikadi pamoja na vionjo vyao.
Hivyo,
majazi ambayo mtunzi anawapa wahusika majina kulingana na tabia, sifa, dhima na
matendoyao. Hii imetumika katika ukurasa wa 7 na 8.
Mhubirinakichaa
ukurasa wa 7 mpaka ukurasa wa 8.
Zamani
za kale paliishi wakaziwa chache sana na labda watatu. Mmoja
alikuwanimhubirialiyeishi upande wa pili unaoelekeana na machweo ya jua. Nyuma
yake siku hizi imebakia kuwa bandakuu baada ya
mkwewekuondokakwakulalamikachakulakimepotea na
wamebakiakulavyakulavinavyotolewa kama sadaka na waumini. Ukiinamia upande wa
pili kulikuwa na kichaaaliyeishi upande huo katika kibandakilichofanana na kidungu
cha kuwingiandegeshambani; kipompakaleo.
Wanakijijiwanasemakichaahuyoalikuwamgangakabla ya wanakijijikumbatizakichaa.
Mwanasayansi
ukurasa wa 53,
“Baada ya muda
nilimwona yule mwanayansi na wenzake. Walikuwa wakielekea nilikokuwa
nikidhamiria”.
Bina-Adamu
Msafiri ni mhusika mkuu katika riwaya hii ambaye alikuwa akisafiri kutafuta
ufumbuzi wa jambo kusuhusiana na kijiji chao. Hii imejidhihirisha katika ukurasa
wa 34:
“Wewe ni ndiye
Bina-Adamu Msafiri?”
“Ehhh…”
“Tulijua utapita hapa!”
“Mliambiwa na nani?”
“Na babu yako”
Hii
pia imejitokeza katika ukurasa wa 86. Mbinu hii humsadia msomaji kupata dhamira
na ujumbe kwa urahisi zaidi.
Kwa
ujumla riwaya hii ya Bina-Adamu, imefanikiwa kufikisha ujumbe kwa kupitia
vipengele vya fani na maudhui. Kwa mfano katika dhamira ametoa dhamira ambazo
zipo katika jamii yetu ya kiafrika. Dhamira hizi ni kama vile ubaguzi wa rangi,
uongozi mbaya, unyonyaji, historia na uhistoria, ukandamizwaji wa nchi za
Afrika unaofanywa na nchi za Magharibi. Vipengele vya mielekeo chomozi ya
kifani vilivyotumika katika riwaya ya Bina-Adamu
ni muhimu sana katika kukikamilisha kipengele maudhui.
MAREJELEO
Madumulla, J.S
(2009) Riwaya ya Kiswahili: Nadharia,
Historian a Misingi ya Uchambuzi,Sitima Printers and Stationers Ltd,
Nairobi, Kenya.
Msokile, M.
(1992) Nadharia za Uhakiki wa Fasihi; TUKI,
Dar es Salaam.
Senkoro,
F.E.M.K. (2011) Fasihi: Mfululizo wa Lugha na Fasihi, Kitabu cha
Kwanza, KAUTTU, Dar es Salaam.
TUKI (2010) Kamusi ya Kiswahili Sanifu; TUKI, Dar es
Salaam.
Wamitila, K. W.
(2002) Bina-Adamu; Phoenix Publishers
Ltd, Nairobi.
Wamitila, K.W.
(2006) Uhakiki wa Fasihi: Misingi na
Vipengele Vyake, Phoenix Publishers Ltd, Nairobi.
Wamitira, K. W.
(2003) Kamusi ya Fasihi;Istilahi na
Nadharia, Nairobi Focus Publishers, Nairobi.
CASINO CASINO RESORT, LAS VEGAS - Mapyro
ReplyDeleteCasino, 문경 출장안마 Hotel and 경상북도 출장샵 RV Park 안산 출장샵 in 통영 출장안마 Las Vegas (NV). 삼척 출장안마 Get directions, reviews and information for CASINO RESORT in LAS VEGAS.